Monday, March 12

Rais Nkurunziza kuongoza maisha chama tawala


 Mkutano mkuu wa chama tawala cha CNDD/FDD umemtangaza Rais Pierre Nkurunzinza kuwa kiongozi wake wa maisha.
Taaarifa fupi ya Chama cha CNDD/FDD imesema vikao vya chama vilivyofanyika kwa siku tatu mfululizo vililenga kuimarisha chama tawala na taasisi zake na moja ya mambo waliyoona yanafaa ni kumwongezea hadhi na kumpa cheo cha juu Rais Nkurunziza.
Wajumbe wa mkutano huo walifikia uamuzi huo baada ya vikao vya chama vilivyofanyika eneo la Buye Kaskazini mwa nchi ambako ndiko alikozaliwa Nkurunziza.
Tangazo hilo la CNDD/FDD limetolewa wakati Burundi inajiandaa kwa kura ya maoni kuhusu Marekebisho ya Katiba Mei. Kati ya mambo mengi, katiba hiyo ikipitishwa itamwezesha Rais Nkurunzinza kuwania urais mpaka mwaka wa 2034.
Kwenye hafla na makundi ya utamaduni ya chama tawala, katibu mkuu wa CNDD/FDD, Evariste Ndayishimiye aliutangazia umati azimio hilo alilolitaja kuwa ni muhimu mno katika uhai wa chama tawala.
Wadadisi wengi wa siasa za Burundi wanaamini kuwa hatua hii ya chama tawala inakusudia kumaliza mapema mjadala wa mtetezi wa kiti cha urais kupitia chama hicho na kuonyesha mustakabali wa uongozi kabla hata uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2020.
Lakini pia uamuzi huo unapeleka ujumbe kwa wafuasi wa CNDD/FDD na hasa viongozi wenye nia pengine ya kuwania nafasi hiyo na hivyo kujaribu kukiepusha chama tawala na mpasuko kama ilivyotokea mwaka 2015 kuhusu muhula wa sasa wa Rais Nkurunzinza.

No comments:

Post a Comment