Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga walipokutana ghafla Ijumaa na kuahidi kuweka kando tofauti zao kwa maslahi ya taifa, hilo lilitazamwa na wengi kama ishara ya mwisho wa wingu la siasa ambalo limegubika taifa hilo tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Bw Kenyatta na Bw Odinga waliitana "ndugu" na wakakubaliana kuundwe mpango wa pamoja wa kuangazia utekelezaji wa malengo ya pamoja ya viongozi hao wawili, ambao utazinduliwa rasmi karibuni.
"Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu," alisema Bw Kenyatta baada ya mkutano huo, akisisitiza kauli ya Bw Odinga kwamba "Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja."
Katika mkutano wao, kuna wahusika ambao hawakuwepo ambao wengi walisubiri kusikia kauli yao.
Katika Muungano wa National Super Alliance (Nasa) ambao ulibuniwa mwaka jana, Bw Odinga alikuwa na viongozi wengine wa vyama vya upinzani, hususan makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka ambaye ni kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement of Kenya Musalia Mudavadi wa Amani National Congress (ANC) na Moses Wetangula wa chama cha Forum for the Restoration of Democracy-Kenya (Ford-Kenya).
Wote wamekuwa viongozi wenza wa muungano huo.
Punde baada ya mkutano huo kufanyika, walikutana na kutangaza kwamba hawakuwa na habari kuhusu mkutano huo wa bw Odinga na Bw Kenyatta.
Kwenye taarifa ya pamoja, walisema hawana ufahamu kuhusu iwapo mazungumzo hayo ni sehemu ya mazungumzo ambayo Nasa, kama muungano wa siasa, umekuwa ukishinikiza kwamba yanafaa kufanyika kati ya serikali na upinzani.
"Asubuhi ya tarehe 9 Machi 2018, tuliona kwenye vyombo vya habari mkutano kati ya Bw Uhuru (Kenyatta) na Bw Raila Amolo Odinga...Ingawa tumekuwa tukisisitiza mazungumzo yafanyike, sisi kama viongozi wenza wa Muungano wa Nasa, hatukuwa na ufahamu kuhusu majadiliano hayo yaliyofanyika Jumba la Harambee (Afisi ya Rais)," taarifa yao ilisema.
Taarifa kwenye vyombo vya habari kenya zinasema Bw Odinga hajazungumza na viongozi wenzake watatu kuhusu yaliyojadiliwa katika mkutano wake na Bw Kenyatta Ijumaa.
Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye ni katibu mkuu wa chama cha ODM chake Bw Odinga aliingia kwenye mitandao ya kijamii kujaribu kuondoa utata ambapo aliahidi wafuasi wa chama hicho kwamba wana imani na uongozi wa chama hicho.
Mchanganuzi wa masuala ya siasa Kenya anayeegemea upande wa upinzani Prof Makau Mutua pia alionekana kuunga mkono mkutano huo.
Lakini mshauri wa zamani wa Bw Odinga ambaye alitia idhini hati yake ya kiapo alipojiapisha kuwa 'Rais wa Wananchi' mwezi Januari na akafurushwa Kenya na serikali na kupelekewa Canada alieleza hatua hiyo ya Bw Odinga kama "usaliti".
"Hauwezi kuwa na mazungumzo na mtu ambaye hamko katika ngazi sawa," alisema.
Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula walikuwa wamedokeza kwamba wangetafuta ufafanuzi zaidi kuhusu mazungumzo ya Ijumaa wakati wa mkutano mkuu wa muungano huo ambao ulikuwa umepangiwa kufanyika leo Jumatatu.
Dalili za mgawanyiko zilianza kuonekana pale taarifa za vyombo vya habari zilipodokeza kwamba kulikuwa na uwezekano Bw Odinga angesusia mkutano huo.
Lakini Bw Odinga amefika kwa mkutano huo unaofanyika Athi River.
Wakenya sasa, na zaidi wafuasi wa upinzani, wanasubiri kusikia taarifa ya viongozi hao baada ya mkutano wao.
Matukio makuu mzozo wa kisiasa Kenya
- 8 Agosti, uchaguzi mkuu wafanyika ambapo Bw Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi
- 1 Septemba, Mahakama ya Juu yabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta katika kesi iliyowasilishwa na Bw Raila Odinga, na kuagiza uchaguzi urudiwe
- 26 Oktoba, uchaguzi wa marudio wafanyika, huku upinzani ukisusia. Bw Kenyatta atangazwa mshindi.
- 30 Januari, Bw Odinga ala kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kwamba hatambui Bw Kenyatta kama rais halali wa Kenya
- 9 Machi, Bw Kenyatta akutana na Bw Odinga katika afisi ya rais Jumba la Harambee, wawili hao waahidi kushirikiana kuwaunganisha Wakenya.
Kushinikiza mageuzi
Bw Odinga alisusia kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika 26 Oktoba mwaka jana akishinikiza mageuzi yafanywe kwanza katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Uchaguzi huo ulitokana na hatua ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ikisema ulikuwa na kasoro nyingi.
Mahakama hiyo ilikuwa inatoa uamuzi katika kesi iliyokuwa imewasilishwa na Bw Odinga kupinga matokeo hayo.
Bw Kenyatta alishinda uchaguzi huo wa marudio kwa kura 7.5 milioni ambazo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Idadi ya waliojitokeza ilikuwa ni asilimia 38.84 ya waliokuwa wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo.
Uchaguzi ulitatizika sana katika maeneo yenye wafuasi wengi wa upinzani. Katika majimbo manne magharibi mwa Kenya ambayo ni ngome ya Bw Odinga, uchaguzi uliahirishwa kwa siku kadha na baadaye haukufanyika.
No comments:
Post a Comment