Harare, Zimbabwe. Rais wa zamani Robert Mugabe, mwenye umri wa miaka 94, ameelezea masikitiko yake "namna alivyong’olewa madarakani," akisema hayuko tayari kukutana na mrithi wake Rais Emmerson Mnangagwa kwa mazungumzo.
Mugabe alisema hayo wakati mpasuko kati yake na Mnangagwa ukidaiwa "kuongezeka".
Kwa mujibu wa gazeti binafsi la Standard, Mugabe ameapa kwamba hawezi kujadiliana na Mnangagwa kufikia "maridhiano".
Utawala wa miaka 37 wa Mugabe ulifikia kikomo Novemba 15 baada ya operesheni ya kijeshi, ambayo baadhi ya watu waliisifu kama "marekebisho yasiyo ya umwagaji damu".
Mzee huyo, hivi karibuni, aliripotiwa kwamba alikuwa akiunga mkono chama kipya kiitwacho National Patriotic Front (NPF) kinachoongozwa na waziri wa zamani Ambrose Mutinhiri.
Mutinhiri, mkongwe wa vita vilivyopiganwa miaka ya 1970 dhidi ya utawala wa wachache, alikutana na Mugabe wiki chache zilizopita kabla ya kutangaza kwamba alikuwa ameunda chama kipya.
Gazeti la The Standard lilimnukuu Mutinhiri mwishoni mwa wiki akisema haoni uwezekano wa Mugabe na Mnangagwa "kupikika katika chungu kimoja".
Mutinhiri ameripotiwa akimnukuu Mugabe akisema: "ED (Mnangagwa) anafikiri mimi ni zuzu.
"Anawezaje kufikiri kwamba naweza kuamini madai yao kwamba wanalinda heshima ya rais, urithi wangu, wakati niko chini kwa sababu yao huku wakiniburuta kwenye matope?
"Watu, hasa ndani ya Zanu-PF, wanataka viongozi waaminifu wa kulinda urithi wa rais na wanasema wanalaani unafiki, wanashutumu ukatili wa kijeshi dhidi ya watu.
"ED anasema ananitaka nimwidhinishe, nitakuwa naidhinisha nini? Unafiki? Ukatili dhidi ya watu?
Matamshi hayo yamekuja baada ya gazeti hilo la kila siku kusema mwishoni mwa wiki kuwa waziri wa zamani wa serikali ya Mugabe alimshawishi mkongwe huyo wa siasa kukutana na Mnangagwa katika juhudi za kusawazisha mambo.
Mpango huo, ripoti hiyo imesema, ulihusu kumweka Mugabe kama “mzee” wa chama tawala ili kumuunga mkono Mnangagwa.
No comments:
Post a Comment