Monday, March 12

Naibu Waziri ahimiza Watanzania kupima afya zao

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile amewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka ili kubaini kwa haraka endapo ugonjwa utaingia mwilini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 12, 2018, Dk Ndugulile amesema watu wengi wamekuwa wakiathirika na kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa matibabu kwa wakati.
“Magonjwa kama kisukari, kiharusi, shinikizo la damu, shinikizo la macho yamekuwa yakiongezeka sana lakini watu wanashindwa kuyabaini mapema kwa sababu hawana utamaduni wa kufanya vipimo mara kwa mara,” amesema.
Amesema ugonjwa huo una athari kubwa unapoingia kwenye macho ya binadamu lakini wengi hawafahamu kwa sababu unaingia taratibu na si rahisi kuonekana kwa haraka.
Kwa mujibu wa Dk Ndugulile takribani watu 1,740,000 nchini wana matatizo ya kutoona vizuri lakini kwa mwaka 2017 watu 13,420 pekee ndiyo walihudhuria kwenye vituo vya afya wakiwa na tatizo la shinikizo la macho.
Takwimu za Shirika za Afya Duniani (WHO) zinaonyesha ifikapo mwaka 2020 idadi ya watu wasioona kutokana na ugonjwa wa shinikizo la macho itafikia 11.2 milioni.
Amesema waathirika wakubwa wa ugonjwa huo ni watu wenye umri kuanzia miaka miaka 40 na kwa kiasi kikubwa husababisha upofu.
Dk Ndugulile amewataka wananchi kutumia maadhimisho ya siku ya afya ya macho yaliyobebwa na kauli mbiu ‘Okoa uoni wa macho yako’ kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kupata vipimo na tiba.
“Ukiwahi ugonjwa huu katika hatua za mwanzo uwezekano wa kupona ni mkubwa sana, niwasihi Watanzania wapime afya zao na ukiona una dalili zozote kwenye macho yako ni vyema ukaenda hospitali kabla ya kufikia kwenye upofu,”
“Mwaka huu hatutakuwa na yale maadhimisho ya kutoa huduma za wazi hizo fedha ni bora zitibu watu vituoni, kwa hiyo tumieni wiki hii kuanzia Machi 11 hadi 17 kwenda kwenye vituo vya afya,” amesema Dk Ndugulile

Dondoo
Watu 253 milioni wana tatizo la kutoona vizuri
Kati yao watu 36 milioni hawaoni kabisa
Ifikapo 2020 idadi ya watu wasiiona kutokana na shinikizo la macho inakadiriwa kufikia 11.2 milioni.

No comments:

Post a Comment