Monday, March 12

JPM: Serikali itapunguza maeneo ya hifadhi kuwapa wananchi

Rais John Magufuli akiwawapungia mkono  wana
Rais John Magufuli akiwawapungia mkono  wana kwaya wa Baraka wakati alipowasili Uyovu kwa ajili ya ufunguzi wa barabara ya Uyovu- Bwanga iliokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami katika eneo la Uyovu mkoani Geita jana .Picha na Ikulu 
Rais John Magufuli amesema kutokana na ongezeko kubwa la watu nchini, Serikali inajipanga kuangalia namna bora ya kupunguza maeneo ya hifadhi na kuyagawa kwa wananchi.
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Barabara ya Uyovu - Bwanga, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita yenye urefu wa kilomita 45 iliyojengwa kwa kiwango cha lami kwa Sh47.95 bilioni, Rais Magufuli alisema takwimu zinaonyesha kuwa Watanzania wameongezeka kutoka milioni 10 wakati nchi ikipata Uhuru mwaka 1961, hadi watu milioni 54, mwaka 2017/18.
Huku akiwataka Watanzania na mamia ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo kuipa Serikali muda ili iweze kujipanga, alisema wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya 300,000 na kuna pori la akiba la Kigosi Muyowosi ambalo asilimia 40 tu ndio hutumiwa na wananchi.
Wakati Rais akizungumzia suala la kupunguza maeneo ya hifadhi na kuwagawia wananchi, baadhi ya wananchi walisimama wakiwa na mabango wakidai maeneo ya kilimo na ufugaji.
“Kabla sijaona mabango yenu nilishapanga kuzungumza hili kwa hiyo shusheni mabango kilio chenu nakijua, siwezi kuwatupa na nyie msinitupe kwa kufanya fujo, ipeni Serikali muda lazima tupunguze maeneo,” alisema Rais Magufuli.
Wananchi wa Wilaya ya Bukombe wamekuwa na kilio cha muda mrefu kwa Serikali wakiomba kuongezewa eneo kutoka kwenye pori la akiba kutokana na wakazi wake kutokuwa na maeneo ya ufugaji na kilimo.
Rais Magufuli alizungumzia uchumi na kubainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake umekua na kuwataka Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwapuuza wale ambao hawaoni kazi inayofanywa.
Alisema Tanzania haipaswi kuwa nchi ya kuombaomba kwa kuwa ina utajiri mwingi na kusema sheria mpya ya madini itazalisha fedha za kutosha za kuwahudumia Watanzania.
Alisema wakati anaingia madarakani, sekta ya afya ilikuwa inatengewa bajeti ya Sh31 bilioni, lakini ameipandisha na kwamba mwaka huu imeongezeka hadi kufikia Sh269 bilioni lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Kuhusu elimu, alisema zaidi ya Sh23.8 bilioni hutolewa kila mwezi kwa ajili ya utekelezaji wa elimu bure na kwamba wanafunzi 125,000 wa elimu ya juu wamepatiwa mikopo ambayo imegharimu Sh483 bilioni.
Amani
Rais Magufuli alisema wapo wasiopenda kuona Tanzania ikidumu katika utulivu huku akiahidi kuilinda amani iliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na kuenziwa na watangulizi wake kwa zaidi ya miaka 50. Alisema kuna kundi halifurahishwi na mafanikio yanayoonekana ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa, hospitali, barabara za lami na Tanzania kuwa na umeme kila mahali. “Vijana, kina mama tuibebe hiyo amani kwa faida ya Tanzania nzima, Taifa letu kwa zaidi ya miaka 50 limekaa na amani, msifikiri wengine wanafurahi, wangependa nchi isiwe na amani na isambaratike, tunayoyafanya kwa nchi yetu ni makubwa,” alisema.
Katika mkutano huo, uliofanyika Lunzewe wilayani Bukombe, Rais Magufuli wakati mwingine alitumia maneno ya lugha ya Kisukuma kusisitiza ujumbe wake kwa mamia ya wananchi waliokuwa wamejitokeza kumsikiliza.
“Kwa ustawi wa nchi yetu hawawezi kufurahi, tuwazuie dhahabu wafurahi wakati walikuwa wanasomba tu? Tutengeneze reli ambayo ilijengwa miaka 112 iliyopita, leo tunajenga reli kutoka Dar es Salaam-Dodoma mpaka Lusumo, reli ya umeme, spidi 160 kwa saa, mizigo mingi nani afurahi? Nani afurahi kuwajengea hospitali hawa kina mama?” Alihoji.
“Nani afurahi kuona barabara za lami zinajengwa, nani afurahi Tanzania kuwa na umeme kila mahali wakati nchi zingine hazina umeme, nani afurahi Tanzania kuwa na mitandao ya simu kila mahali, nani afurahi nchi hii kuwa na amani, maendeleo hayana chama.
“… Amani ni kitu muhimu, hata mitume walihubiri amani, Yesu aliwaambia nawaachieni amani, kwa hiyo nawaambia amani tuliyonayo imejengwa na Mwalimu (Nyerere), amekuja (Ali Hassan) Mwinyi, amekuja (Benjamin) Mkapa, amekuja Jakaya (Jakaya) ameitunza amani hiyo,” alisema.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria uzinduzi huo ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, Katibu Mkuu wizara hiyo, Joseph Nyamhanga, Mbunge wa jimbo hilo, Dotto Biteko na watendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

No comments:

Post a Comment