Jengo hilo la shule ya Green Acres lina madarasa ya wanafunzi wa msingi na sekondari.
Nyumba nyingine zinazotarajiwa kukumbwa na hatua hiyo ni za kata za Bunju, Mabwepande, Makongo na Wazo.
Wakazi hao wamelalamikia hatua ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) kuwataka kubomoa nyumba zao wakisema sheria inaelekeza nyumba zianze kujengwa mita tano baada ya bomba lakini wanashangaa kuambiwa walio ndani ya mita 15 waondoke.
Mwandishi wetu aliyefika katika eneo la Salasala jana, alikuta nyumba na majengo kadhaa yakiwa yamewekewa alama nyekundu iliyoandikwa ‘DAWASA’ ikionyesha eneo linalotakiwa kubomolewa.
Akizungumzia hatua hiyo, mkurugenzi wa Green Acres, Dk Julian Bujugo alisema ni kinyume na sheria, wanalenga kuwaonea wananchi ambao wametumia nguvu kubwa kujenga nyumba zao.
Alisema sheria inataka watu wawe umbali wa mita tano kutoka lilipo bomba lakini wameshangaa kuambiwa wabomoe majengo yao yote yaliyo ndani ya mita 15.
“Ukisoma sheria na kitabu cha mradi unaona wazi Dawasa wanaonea wananchi, nia yao ni kutaka kumharibia Rais na Serikali yake,” alisema na kuongeza: “Tunamuomba Rais (John) Magufuli aingilie kati suala hili, sisi wananchi tunanyanyasika.”
Alipotafutwa kwa simu kuzungumzia hatua hiyo, meneja uhusiano wa Dawasa, Neli Msuya alisema, “Kama ilivyo kwenye barabara au reli ukiingilia miundombinu hiyo unaondolewa ndivyo ilivyo hata kwenye bomba. Hilo suala lina mambo mengi ukitaka kwa undani na vielelezo vyote njoo ofisini utapata.”
Hata hivyo, mwandishi wetu hakuweza kuona vielelezo hivyo kwa kuwa muda huo ofisi za Dawasa zilikuwa zimefungwa.Mkazi mwingine wa Mbezi Juu, Isaya Mohamed alisema wananchi hawajafahamishwa kama kuna mabadiliko yoyote ya sheria yaliyofanyika akisema wanayoifahamu inaelekeza wawe umbali wa mita tano.
“Huenda sisi ndiyo hatuelewi, mamlaka (Dawasa) ingekuja kutusaidia ni sheria ipi wanayotumia kwa sababu tunayoifahamu inaelekeza mita tano, sasa hizo mita 15 zimetoka kwenye sheria gani? Je, sheria imefanyiwa marekebisho.
“Mara ya kwanza walituwekea mipaka na wakaja kubomoa tunashangaa safari hii wamerudi na mita 15 kinachotushangaza ni kwa nini hawajaja kuzungumza na wananchi? Wao wameweka alama na kuondoka zao.”
Diwani wa Wazo, John Mwakalebela alisema amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi wake. “Hili suala lipo, wananchi wametulalamikia na liliibua mjadala kwenye baraza la madiwani. Ukweli ni kwamba limezua taharuki kwa wengi na hadi sasa hatujui kama wananchi watalipwa fidia au la ila watakokumbwa na athari hii ni wengi.
“Tunafanya mipango ya kukutana na watu wa Dawasa ili watoe ufafanuzi maana imekuwa ghafla watu wamerudi wamekuta nyumba zao zimewekewa alama ya kubomolewa.”
No comments:
Post a Comment