Saturday, March 3

Albino asiye na mikono yote kupanda Mlima Kilimanjaro


Wanawake wenye ulemavu wa ngozi barani Afrika akiwamo Mtanzania aliyekatwa mikono yote miaka 10 iliyopita kwa imani za kishirikina, Mariam Stanford watapanda Mlima Kilimanjaro ili kutoa ujumbe kwa dunia kwamba licha ya ulemavu walionao, wana uwezo wa kufanya jambo lolote.
Mpango huo wa kukwea Mlima Kilimanjaro umebuniwa na mwanaharakati wa haki za binadamu, Jane Waithera na kusimamiwa na Taasisi ya Under the Same Sun (UTSS).
Akizungumza katika mkutano leo Ijumaa, Machi 2, Waithera amesema wanawake hao watapanda kwa siku nane kuanzia Septemba 24, 2018.
Mariam amesema kutokana na changamoto alizozipata, anaona kazi ya kupanda mlima itakuwa rahisi licha ya ulemavu wake.
"Nimekatwa mikono miwili bila ganzi, nimeishi maisha ya hofu, sasa ninajiamini ninaweza kufanya jambo lolote linaloweza kufanywa na binadamu," amesema.
Amesema wanapanda Mlima Kilimanjaro ili, “Kuwaonyesha watu kwamba sisi ni wanawake wenye ulemavu wa ngozi lakini tunaweza.”
Katika kudhihirisha kwamba anaweza licha ya ulemavu wa aina mbili alionao, Mariam anatengeneza masweta ambayo yamekuwa yakimwingizia kipato na kumfanya awe na maisha mazuri.
Mwanzilishi wa taasisi ya UTSS, Peter Ash kutoka Canada amesema wanawake hao kupanda Kilimanjaro kama kielelezo kwamba wanaweza kujitegemea.
"Kupanda mlima ni njia nzuri ya kuwaonyesha watu kwamba tupo, tunajitegemea na tunaweza" amesema.
Mkurugenzi mtendaji wa UTSS, Vicky Ntetema amesema hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa wanawake wenye ulemavu wa ngozi kupanda Mlima Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment