Saturday, March 3

NCAA na Tato kushirikiana kukuza utalii nchini

Naibu Mhifadhi wa NCAA anayeshughulikia  huduma
Naibu Mhifadhi wa NCAA anayeshughulikia  huduma za shirika,  Asangye Bangu 
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Chama cha Mawakala wa Utalii (Tato), wamefikia makubaliano  ya kuondoa vikwazo na tofauti baina yao, hivyo kushirikiana katika kukuza utalii hapa nchini.
Makubaliano hayo, yalifikiwa leo Machi 2, katika kikao kilichofanyika Arusha,   kati ya  viongozi wa NCAA,Tato na  kampuni za utalii  ambazo hivi karibuni zilitajwa kuwa huenda zingezuiwa kuingiza watalii katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Mhifadhi wa NCAA anayeshughulikia  huduma za shirika,  Asangye Bangu amesema  NCAA imejipanga kuboresha huduma kwa watalii na kuondoa changamoto zinazowakabili wenye kampuni za utalii.
"Kikao chetu kimekwenda vizuri, NCAA tutaendelea kuboresha mifumo ya malipo, kuboresha mawasiliano baina yetu na mawakala wa utalii lakini pia kutatua changamoto kadhaa, ikiwamo barabara ndani ya hifadhi,"amesema
Bangu amesema katika kukabiliana na kero ya barabara, Agosti 8 mwaka huu NCAA inatarajiwa kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka geti la kuingia Ngorongoro hadi la Serengeti lenye urefu wa kilomita 83 kwa kuweka tabaka gumu juu.

"Hii ni kero ya muda mrefu ya kampuni ya utalii lakini sasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) limetukubalia kuijenga barabara hii na ikikamilika tuna imani barabara itadumu kwa zaidi ya miaka 40,"amesema.
Awali, Katibu Mtendaji wa Tato, Siriri Akko amesema katika siku za karibuni kuliibuka taarifa za kuwachanganya baadhi ya wanachama wao juu ya kuzuiwa kuingia Ngorongoro kupeleka watalii.
Hata hivyo, amesema baada ya kupata maelezo kutoka NCAA wamefikia makubaliano ambayo lengo lake ni kuboresha sekta ya utalii nchini na pia kuondoa changamoto zinazowakabili.
"Kikao chetu kimekwenda vizuri na ile hofu ya kampuni kuzuiwa sasa haipo na tuna imani kampuni zote zitafuata sheria na taratibu za kufanya biashara ya utalii hapa nchini,"amesema.
Akizungumza katika kikao hicho leo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Shidoria, Lazaro Mafie amesema ni muhimu kuwapo na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya NCAA na kampuni za utalii ili kutatua kero.
Mafie amesema wao kama wamiliki wa kampuni za utalii, wateja wao ni watalii sawa na NCAA ambayo uwapo wao unategemea watalii, hivyo ni lazima kuwapo na mawasiliano mazuri baina yao.
"Kuna changamoto kadhaa ambazo tunakabiliana nazo lakini tuna imani sasa zitafanyiwa kazi ili kuboresha sekta ya utalii hapa nchini,"amesema.

No comments:

Post a Comment