Monday, December 4

Wanafunzi UDSM wazungumzia nyufa majengo mapya ya hosteli

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wameingia hofu baada ya mabweni wanayoishi kuwa na nyufa.
Mabweni hayo yanayotumiwa na wavulana katika jengo la Block A yana nyufa sehemu mbalimbali kuanzia chini hadi ghorofa ya tatu.
Akizungumza na MCL Digital mbunge wa serikali ya wanafunzi (Daruso), Simon Masenga amesema nyufa hizo zilianza kuonekana wiki mbili zilizopita.
Amesema walitoa taarifa kwa meneja wa hosteli lakini majibu waliyopewa ni kuwa majengo hayo yako chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Mbunge mwingine wa serikali ya wanafunzi, Kumbusho Dawson amesema leo Jumatatu Desemba 4,2017 kuwa majengo hayo yana upungufu, ukiwemo wa maji kutuama kwenye bafu na kutokuwa na makabati.
"Tumelalamika kwa meneja wa mabweni kuhusu upungufu katika majengo haya na majibu tunayopewa ni kuwa bado yako chini ya TBA," amesema Dawson.
Majengo hayo yaliyojengwa na TBA kwa miezi minane yakielezwa kugharimu Sh10 bilioni yalizinduliwa Aprili 15,2017.
Ujenzi ulifanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kumaliza tatizo la malazi kwa wanafunzi wa UDSM.
Picha zinazoonyesha nyufa kwenye majengo hayo zilianza kusambaa mitandaoni jana Jumapili Desemba 3,2017.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga akizungumza na MCL Digital jana Jumapili alisema naye aliziona picha hizo kwenye mitandao ya kijamii.
“Nimeziona na muda huu najiandaa kwenda huko kuangalia kama taarifa hizo ni za kweli,” alisema Mwakalinga alipozungumza na MCL Digital saa mbili usiku na kuahidi kutoa taarifa baada ya kukagua majengo hayo.
Kwa mujibu wa wanafunzi waliozungumza na MCL Digital, maofisa wa TBA walifika kwenye hosteli hizo maarufu kwa jina la Hosteli za Magufuli jana usiku na kufanya ukaguzi.
Baadhi yao inaelezwa walilala katika eneo hilo kwa ajili ya uchunguzi na hata walipofuatwa na uongozi wa serikali ya wanafunzi hawakuwa tayari kuzungumza lolote.

No comments:

Post a Comment