Monday, December 4

Serikali yashauriwa kuboresha sheria ya uvuvi


Mtwara. Serikali imeshauriwa kuboresha sheria ya uvuvi ili kuwabana wote wanaojishughulisha na uvuvi haramu wa kutumia milipuko.
Imeelezwa kutokana na sheria kutotoa adhabu kali kwa watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani hulipa faini na kuendelea na shughuli zao, hivyo kupunguza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya Taifa.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu Desemba 4,2017 mkoani Mtwara wakati wa kikao cha utambulisho wa mradi wa kukabiliana na uvuvi wa milipuko ulioandaliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira na Maendeleo ya Jamii (WWF).
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda amesema kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kwa kushirikiana na wadau wamedhibiti uvuvi haramu wa kutumia milipuko lakini baadhi ya watu wachache wamekuwa wakiendelea na hata wanapofikishwa mahakamani wanaishia kulipa faini.
Mmanda amesema uvuvi haramu umeleta matatizo mengi ambayo hayakuwepo, ikiwa ni pamoja na kuharibu mazingira ya bahari, soko la samaki nje ya nchi na umasikini kwa jamii.
"Kuna watu wanajishughulisha na uvuvi haramu, mwingine hata akifikishwa mahakamani anakuja tayari ana faini mfukoni analipa anarudi kuendelea na uvuvi ili arudishe fedha aliyolipia faini," amesema Mmanda.
Mtendaji wa mradi wa WWF, Thomas Chale amesema uvuvi wa kutumia milipuko umepungua ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.
Amesema huo mkoani Mtwara kwa sasa uvuvi wa kutumia milipuko unafanyika mara moja kwa wiki na wakati mwingine haufanyiki kabisa lakini kwa maeneo ya Kigamboni na Masaki jijini Dar es Salaam bado unafanyika.
"Maeneo ya Kilwa kwa siku walikuwa wanasikia milipuko 20 lakini sasa unaweza usisikie kabisa au mmoja kwa wiki,” amesema.
Mkutano huo umewashirikisha wadau kutoka Kilwa, Lindi na Mtwara.

No comments:

Post a Comment