Wednesday, December 6

Maandalizi sherehe ya miaka 56 ya Uhuru yaiva


Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru yamefikia hatua za mwisho huku Serikali ikieleza kuwa sherehe hiyo itapambwa na gwaride la mkoloni litakalofanywa na Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema
itakuwa ni mara ya kwanza kwa gwaride hilo la mkoloni kufanyika katika sherehe hiyo ambayo mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.
“Maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na marekebisho ya uwanja na mahitaji mengine muhimu yapo katika hatua za mwisho,” alisema DK Mahenge.
Alifafanua kuwa maonyesho hayo yatakayofanyika Desemba 9 yatajumuisha gwaride maalumu la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini na onyesho la makomandoo.
Nyinginie ni kwata ya kimya kimya iliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Onyesho la Jeshi la mkoloni kutoka Jeshi la Polisi.
“Watoto 225 kutoka shule za sekondari watashiriki katika gwaride hilo,” alisema.
Alisema lengo la Serikali kuwashirikisha ni kuwafundisha na kuwaridhisha tunu ya uhuru, uzalendo, umoja, mshikamano na utaifa.
Pia, kutakuwa na vikundi vya ngoma za asili kutoka Ruvuma, Kigoma, Zanzibar pamoja na kwaya kutoka Chunya mkoani Mbeya.
DK Mahenge aliwasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli kupiga vita rushwa na kufanya kazi kwa bidiii kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Pia, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kutoogopa mizinga itakayopigwa katika sherehe hizo kwasababu haina madhara.

No comments:

Post a Comment