Huwezi kusikia matukio makubwa ya kisiasa sasa kama mikutano mikubwa au midahalo ya kutafuta suluhu za matatizo ya nchi. Habari zote ni fulani kahama pale kahamia hapa.
Baadhi ya wanasiasa ambao walihama vyama vyao vya awali miaka miwili iliyopita ndiyo waliorudia safari hii.
Maulid Mtulia aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni wiki mbili zilizopita hayupo tena CUF sasa ni kada wa chama tawala na ubunge wake umetoweka. Lazaro Nyalandu moja ya makada maarufu wa CCM na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa Serikali ya awamu iliyopita naye ameshahamia Chadema.
Wakati unatafakari ni kiongozi gani wa chama au wa kuchaguliwa kutoka ngazi ya tawi hadi Taifa atakayehama kesho, zipo fununu kuwa kuna wabunge wengine watavitema vyama vyao hivi karibuni kwenda kwingine.
Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma aina ya kuhama kwa sasa kuna nyanja nyingi za kutazama ili kupata mustakabali wa siasa na ukuaji wa demokrasia na maendeleo ya nchi. Baadhi ya mambo ya awali kuyaangazia ni sababu za kuhama, aina ya watu wanaohama na athari wanazoziacha kwa Taifa.
Kipindi wanachohama
Kulikuwa na utamaduni wa miaka ya hivi karibuni kwa watu kuhama vyama baada ya kutokea msigano ndani ya chama ama baada ya majina yao kukatwa katika kuwania nafasi fulani. Kama siyo hivyo basi mwanasiasa huyo ameng’olewa kwa tuhuma mbalimbali kama usaliti.
Pia kuna aina ya kuhama tuliishuhudia mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu baada ya vigogo kuhama vyama. Kumbukumbu kubwa ni uamuzi mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowassa na Frederick Sumaye kuhamia Chadema.
Sehemu kubwa hawa walionekana wazi kuumizwa na mchakato wa uchaguzi. Kulikuwa na watu wengi wa aina hii waliohama vyama vyao au kuachana navyo bila kuhamia sehemu nyingine kama ilivyokuwa kwa Dk Willibrod Slaa aliyetangaza kuachana kabisa na siasa.
Lakini, safari hii wanasiasa wanahama katikati ya safari ikiwa ni miaka miwili baada ya uchaguzi.
Mbaya zaidi wapo wanaohama wakiwa na vyeo vyao vya kuchaguliwa, jambo linalofanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuitisha uchaguzi mdogo.
Sababu za kuhama
Ukiwasikiliza wengi waliokuwa wanahama CCM wakati huo ilikuwa ni kwamba kulikuwa na ufisadi uliokithiri na kwamba kwa mfumo uliokuwapo wasingeweza kufanya mabadiliko wakiwa ndani. Ilikuwa ndiyo sababu kuu ambayo hadi sasa imebaki.
Wachache waliokuwa wakiondoka vyama vya upinzani walijitetea kutokuwepo mfumo imara wa kiuongozi ndani ya vyama.
Hata hivyo, ukichambua kwa kina kwa sasa wanaohamia CCM kutoka upinzani wana sababu zinazofanana kana kwamba kuna mtu kaandika barua ya mfano ambayo wote wanapaswa kuifuata.
Sehemu kubwa ya wanaobwaga manyanga kutoka vyama vya upinzani wamevutiwa zaidi na utendaji wa Serikali ya Rais John Magufuli.
“Nimebaini kuwa Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo sisi upinzani tuliahidi kuyatekeleza,” alisema Mtulia wakati wa kujiuzulu.
Athari kwa Taifa
Moja ya maswali mengi ambayo huenda wengi wanajiuliza ni iwapo kuhamahama kuna faida kwa Taifa.
Jambo la msingi hapa la kufahamu katika suala hili ni kwamba kuhama kupo kikatiba. Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya mwaka 1977 inaeleza uhuru wa “mtu kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au masilahi yake au mengineyo.”
Kwa muktadha huo kuhama chama si dhambi na wala si kosa kwa kuwa ni uhuru wa mtu kujiunga na chama anachotaka.
Suala la msingi ni iwapo kuhama huko kutakuwa na tija katika kujenga msingi wa demokrasia hususan ndani ya chama na iwapo kutahusisha gharama ambazo zitafanya Serikali itumie fedha za walipakodi.
Je, kasi ya watu kuhama vyama vya siasa ina tija kwa mustakabali wa siasa nchini? Hili ni swali linalohitaji mjadala. Hata hivyo, kuna haja ya kufanya utafiti wa kina kuona kama vyama vinanufaika na watu hao wanaohamia.
Ukiachana na sifa za kisiasa ambazo vyama vinavyowapokea watu huzipata, kuna maswali ya msingi yanayoweza kusaidia utafiti huo.
Mosi, watu wote waliohama vyama baada ya kuhamia kwenye vyama vipya walifanya nini? Ni wangapi wamesaidia mabadiliko na wangapi waliendelea kuwa mizigo?
Je, wote wana sifa kama za Zitto aliyeanzisha ACT na kuwaletea kiti cha kwanza cha ubunge au enzi za John Shibuda ambaye alipata ubunge baada ya kuhamia Chadema akitoka CCM?
Mbali na mchango wa ndani ya chama, walifanya nini katika kukuza demokrasia na maendeleo ya nchi baada ya kuingia kwenye chama kipya.
Mchango wa David Kafulila akiwa mwanachama na mbunge wa NCCR-Mageuzi wa kuchochea uwajibikaji katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, ulifanana na alipokuwa Chadema? Ndani ya chama chake kipya—CCM Kafulila ataweza kuibua au kuchochea uwajibikaji?
Vipi kuhusu Nyalandu kuingia Chadema. Kama alishindwa kushawishi mabadiliko akiwa moja ya vigogo ndani ya chama tawala, ataweza kuchochea mabadiliko ya kitaifa akiwa upinzani ambao kwa sasa wanasubiri mikutano ya uchaguzi mdogo au mikutano na wanahabari kupaza sauti zao?
Kujadili mwenendo wa wanaohama vyama kwa sasa bila kujibu sehemu ya maswali kama hayo ni kujifanya tunaona wakati tupo gizani. Tusipokuwa makini huenda ikawa chachu ya kuua vyama na demokrasia siku zijazo iwapo utafiti wa kina hautafanyika.
Ukiachana na manufaa ya wanaohama kwa chama na Taifa, kuna gharama za ziada ambazo walipa kodi tunaziingia ili kutimiza matakwa ya watu tulioamini wanaweza kutuongoza.
Kwa bahati mbaya sheria zinatutaka tuwachague wakitokea kwenye vyama na hii ni kwa sababu Katiba hairuhusu mgombea binafsi. Hii ina maana kuwa kiongozi wa kuchaguliwa aliyepoteza sifa za uanachama wake basi na yale madaraka tuliyomuamini nayo yametoweka.
Vyama vimekuwa na nguvu kuamua hatma ya wale tuliyowachagua. Matokeo yake Taifa limekuwa likiingia kwenye uchaguzi mdogo kwa sababu tu kiongozi fulani aliondolewa kwa hila na chama chake au kaamua kubwaga manyanga.
Kuna kila dalili kwa sasa, sababu hii inatumika kuwashawishi wanasiasa kuachana na vyama vyao ili kushawishi uchaguzi mdogo kwa kuwa ndiyo kipimo kipya cha vyama vya siasa.
Mwenendo huu umesababisha madiwani wengi kuhama kutoka Chadema wakiwamo watano kutoka Wilaya ya Meru na Monduli mkoani Arusha.
Wakazi wa Meru wamepoteza madiwani wengi nchini kwa mfumo huo wa kuhama chama katikati ya safari. Kumekuwapo na tuhuma za kununuliwa ambazo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inachunguza.
Lakini, ukiachana na viongozi wanaofariki au kushindwa kuendelea na majukumu kutokana na ugonjwa, wanaohama vyama wanawanyonya walipakodi bila sababu ya msingi.
Serikali inaingia gharama kubwa za uchaguzi mdogo kwa sababu yao. Katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 43 hivi karibuni, NEC ilibainisha kuwa ilitumia Sh2.5 bilioni kuukamilisha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhani ni kwamba msingi wa bajeti huo unatokana na vituo vya kupigia kura na idadi ya wapiga kura waliojiandikisha.
Katika uchaguzi huo, ulioisha kwa rabsha katika baadhi ya maeneo nchini kwa baadhi ya watu kujeruhiwa katika vurugu, kulikuwa na vituo vya kupigia kura 884 na wapiga kura 333,309.
Kama uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata 43, Serikali ilitumia Sh2.5 bilioni je ni fedha kiasi gani zitatumika kugharamia uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni, Singida Kaskazini na mengineyo ambayo kuna fununu wabunge wake watahama vyama?
Sh2.5 bilioni ni nyingi kwa hali ya sasa ya kiuchumi na hazitakiwi kufujwa bila sababu za msingi. Ni busara kufanya uchaguzi mdogo kwa matukio makubwa kama ya kifo au ugonjwa ambayo hayawezi kuzuilika.
Fedha hizo zingesaidia kununua dawa katika vituo vya afya au kujenga visima katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji kama Nachingwea mkoani Lindi.
Gharama hizo siyo tu kwa walipakodi bali hata vyama na wagombea wenyewe. Fedha ambazo zingetumika kufanya maendeleo ndani ya chama na kwa wagombea wenyewe zinaishia kugharamia chaguzi za mara kwa mara ambazo msingi wake huenda ni wa kutimiza matakwa ya kisiasa zaidi kuliko kujenga mustakabali wa nchi.
Kuna baadhi watasema demokrasia ni gharama. Ndiyo ni gharama lakini siyo gharama zinazosababishwa kizembe kama za diwani kuchaguliwa leo na kuondoka kesho kwa kutoa sababu za kizembe.
Vyama vyenyewe vinaumia kwa aina hii ya siasa kama ambavyo CUF imeonyesha.
“CUF haikutarajia kuingia katika uchaguzi mdogo hasa jimbo la Kinondoni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 labda kingetokea kifo. Tunawaomba radhi wakazi wa Kinondoni,” Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Abdul Kambaya aliwaambia wanahabari baada ya Mtulia kujiondoa katika chama chao.
Kama hakutakuwa na uchunguzi wa kina kwa wanaohama, huenda Taifa likajikuta kila baada ya miezi mitatu linafanya uchaguzi mdogo kwa kuwa ndiyo itakuwa kipimo kipya cha umaarufu wa kisiasa.
Hata hivyo, kuna njia za kutokomeza tabia hii ya watu kuhamahama kila siku hasa viongozi wanaoongeza gharama kwa Serikali.
Mosi, tumalizie mchakato wa Katiba Mpya. Katiba mpya inaweza kupunguza gharama hizi za kuitisha uchaguzi kwa kuwa mtu kajitoa kwenye chama iwapo itaruhusu mgombea binafsi na kuweka masharti rafiki ya watu kutopoteza nafasi zao hata baada ya kuhama vyama.
Jambo jingine ni kuacha fikra za siasa ya kubomoana na kukomoana. Siasa za kuchekelea kuwa tumeng’oa ‘injini’ muhimu huku mkiwaumiza wananchi, siyo rafiki na hazifai kuwepo kwenye Taifa la wastaarabu kama Tanzania.
Sehemu kubwa wanaohama inaonekana kama ni matokeo ya kwamba tuwakomoe wapunguze viti vya udiwani au ubunge.
Matokeo yake hata huo uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni haujawa na matokeo mazuri kwa demokrasia kutokana na kuwa na mwitikio mdogo na vurugu zilizojitokeza ikiwemo baadhi ya watu kukatana mapanga.
CCM au upinzani wanaweza wakawa wamepata viti vya udiwani katika uchaguzi huo uliopita lakini makovu na majeraha walioyapata Watanzania hao hayafutiki kirahisi na huenda yamezigharimu familia zao. Siasa za namna hii ni mbaya na hazifai kwa kushabikiwa hata kidogo.
Tanzania inaweza kusonga mbele katika siasa ya maendeleo iwapo siasa itafanywa kwa kufuata misingi imara ya demokrasia.
No comments:
Post a Comment