Wednesday, December 6

CWT yataka upandishaji madaraja, vyeo uanze Juni, 2016


Dar es Salaam. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimetaka Serikali kuanza kuhesabu madaraja na vyeo walivyopewa walimu kuanzia Juni, 2016 badala ya Novemba, 2017 kama ilivyotangazwa.
Kazi ya upandishaji madaraja ilitarajiwa kufanyika miezi 19 iliyopita kabla ya kuzuiwa kupisha uhakiki wa watumishi hewa na wenye vyeti feki.
Kaimu Rais wa CWT, Leah Ulaya amesema leo Jumatano Desemba 6,2017 kuwa matarajio yao yalikuwa ni kuona baada ya uhakiki kukamilika madaraja yaendelee kama kawaida kuanzia pale kazi ilipositishwa.
“Tunabaki na swali la kujiuliza, wale walimu waliopandishwa madaraja kati ya Februari na Aprili, 2016 mapunjo na hatima yao ikoje na hasa baada ya agizo hili la madaraja kuanza Novemba Mosi,2017,” amesema Ulaya.
Amesema kuna baadhi ya walimu walioachishwa kazi wakati uhakiki ukiendelea na baadhi wakiwa wameshapata barua za kupandishwa madaraja, hivyo Serikali inatakiwa kuangalia namna ya kuwasaidia.
Ulaya amesema Serikali inapaswa kutoa ufafanuzi wa kutosha kwa walimu ili watambue barua na madaraja waliyopewa awali kama yana maana yoyote.
Amesema kwa kuzingatia hilo, wamepanga kufikisha kilio chao kwa Rais John Magufuli katika kikao kitakachofanyika Desemba 14 na Desemba 15,2017 mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment