Pia, kibanda cha walinzi wa jengo la Tanesco kimevunjwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Uvunjaji huo uliofanyika usiku wa kuamkia jana Jumamosi Desemba 2,2017 ni maandalizi ya kuvunja sehemu ya jengo la ghorofa lenye ofisi za Tanesco eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam ambalo liko kwenye hifadhi ya barabara.
Ubomoaji huo unafanyika pia kupisha utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa barabara za juu eneo la Ubungo.
Meneja wa kikosi cha ujenzi TBA, Humphrey Killo amesema leo Jumapili Desemba 3,2017 kuwa wanafanya maandalizi ya kubomoa jengo la ghorofa.
Amesema wanatarajia maandalizi hayo yatakamilika Jumanne Desemba 5,2017.
Jumanne Novemba 28,2017 akizungumzia kuhusu ubomoaji wa jengo hilo, Kaimu Meneja Uhusiano wa Tanesco, Leila Muhaji alisema wafanyakazi wamehamia katika ofisi zingine za shirika hilo zilizoko jijini Dar es Salaam.
Uongozi wa Tanesco katika taarifa kwa umma iliyotolewa Jumatatu Novemba 27,2017 ulisema umeanza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuhusu kubomolewa jengo hilo.
Novemba 15,2017 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo lenye ofisi za Tanesco sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.
“Katika kipindi hiki cha utekelezaji wa agizo la Rais. Tunapenda kuwahakikishia wateja na Watanzania kwa jumla kuwa, huduma za umeme zitaendelea kupatikana kama kawaida ikiwemo huduma ya ununuzi wa Luku,” imesema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment