Saturday, November 25

WIZARA KUONGEZA WIGO WA MATUMIZI YA KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba leo akiongea na Wanachama wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki (CHAKAMA) amesema Wizara inaendelea na jitihada za kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Nchi Wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo hadi sasa tayari baadhi ya nchi wanachama zimeshaweka lugha ya Kiswahili katika mitaala ya Elimu katika shule za Msingi na Sekondari hatua ambayo itawezesha kuongeza wigo wa matumizi ya lugha hii katika Jumuiya yetu.

Mhe. Dkt Kolimba akizungumza katika kongamano hilo amewapongeza Viongozi na Wanachama wa Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki kwa kuwahusisha baadhi ya Ofisi za Balozi zilipo nchini katika hatua za kufanikisha Kongamono hilo. Kwa namna ya pekee alitumia fursa hiyo kumpongeza Balozi wa Kuwait nchini Mhe.Jaseem Al Najem na Watumishi wa Ubalozi huo kwa kukubamwaliko wa kushiriki Kongamano na kwa mchango waliotoa kufanikisha Kongamano hilo.

Tokea mwaka 2004 hadi sasa Kiswahili kimekuwa lugha ya kwanza ya Afrika kutumika katika vikao vya Ngazi ya Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika, hii ni kufuatia jitihada na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Jitihada hizo ilikuwa ni pamoja na kugharamia wakalimani kwa fedha za ndani, na mwaka 2008 Wizara iliishawishi Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuchukua jukumu hilo.

Aidha Mhe. Dkt. Kolimba amewahakikishia Viongozi na Wanachama wa CHAKAMA kuwa nia ya Serikali ya kufungua vituo vya kufundishia lugha ya kiswahili sehemu mbalimbali nje ya mipaka ya Tanzania bado iko palepale, "tayari tulishafungua kituo kimoja mwaka 2012 katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia" amesema Mhe. Dkt. Kolimba.

CHAKAMA imehitimisha Kongamano lake leo lililofanyika kwa muda wa siku mbili mjini Dodoma ,likiwa na kauli mbiu ya "Kiswahili na Maendeleo ya Afrika Mashariki" chama hiki kinaundwa na nchi Wanchama za Jumuiya ya Afrika pia kinahusisha wanachama kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Ghana na Zimbabwe.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba akihutubia washiriki wa kongamano la Chama cha Kiswahili Afrika Mashariki lililofanyika katika Hoteli ya African Dream mjini Dodoma 
Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba akimkabithi cheti cha ushiriki mmoja wa wajumbe wa Kongamo la CHAKAMA 
Naibu Waziri Mhe.Dkt. Kolimba akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kongamano 

No comments:

Post a Comment