Washambuliaji waliwaua karibu waumini 235 katika shambulizi la bomu na bunduki ndani ya msikiti mmoja uliokuwa umejaa watu katika mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri.
Mlipuko wa bomu uliutikisa msikiti wa al-Rawda, karibu kilometa 40 magharibi mwa mji mkuu wa mkoa wa Sinai Kaskazini, El-Arish, kabla ya watu waliokuwa na silaha kuanza kuwafyatulia risasi waombolezaji wa Kiislamu wa madhehebu ya Sufi waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya maombi ya kila wiki.
Mashuhuda wamesema washambuliaji waliuzingira msikiti huo kwa kutumia magari maalum na kisha wakatega bomu sehemu ya nje. Washambuliaji hao kisha walitumia magari yao kuwakanyaga waumini waliokuwa wakijaribu kukimbia na wakatumia magari ya watu waliyokuwa wameyawasha moto na kuzuia njia za kuingia na kutoka kwenye msikiti huo.
Jeshi la anga la Misri baadaye liliyaharibu magari yaliyotumika katika shambulizi hilo na maeneo ya "kigaidi” ambako silaha zilikuwa zimehifadhiwa, amesema msemaji Tamer el-Refai.
Ofisi ya mwendesha mashitaka wa serikali imesema watu 235 waliuawa na wengine 109 wakajeruhiwa katika shambulizi hilo, ambalo kiwango chake hakijawahi kuonekana katika uasi wa miaka minne unaoendeshwa na makundi ya itikadi kali. Mmoja wa waliojeruhiwa kwenye tukio hilo Magdy Rizk ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kati ya washambuliaji 10 na 20 waliokuwa na silaha waliingia msikitini, na kuwauwa watu Zaidi kuliko waliojeruhiwa. Walikuwa wamefunika nyuso zao na kofia na kuvalia sare za kijeshi.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwenye Twitter kuwa ni "shambulizi la kinyama na la kigaidi dhidi ya waumini wasioweza kujikinga”.
Rais wa Misri aliyekuwa amejawa na hasira Abdel Fattah al-Sisi alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa na kuahidi "kujibu shambulizi hilo kwa kutumia nguvu kali”.
Rais wa Urusi Valdmir Putin alituma salamu za rambirambi kwa Sisi, akililaani shambulizi hilo sawa na nchi za Ujerumani, Uturuki, Italia, Kuwait, Lebanon, Umoja wa Falme za Kiarabu, Israel, Iran, Iraq, Saudi Arabia, Umoja wa Ulaya na nyingine.
Imam mkuu wa msikiti wa Al-Azhar mjini Cairo, Sheikh Ahmed el-Tayeb, alilaani vikali shambulizi hilo la kigaidi na ambalo ni la kinyama.
Hakukuwa na taarifa yoyote ya haraka ya aliyedai kuhusika na umwagaji damu huo mkubwa.
Tawi la MISRI la kundi linalojiitab Dola la Kiislamu limewaua mamua ya polisi na wanajeshi, na pia raia wanaotuhumiwa kushirikiana na mamlaka, katika mashambulizi kaskazini mwa rasi ya Sinai.
Katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg ameliita shambulizi la kinyama wakati Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akiitaja kuwa ni kitendo cha uovu na uwoga.
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amesema shambulizi hilo ni kitendo cha kinyama na kwamba anaomboleza na wahanga.
No comments:
Post a Comment