JESHI la Polisi nchini limesema hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kubaini miili 15 iliyookotwa ikiwa imefungwa kamba katika fukwe za Bahari ya Hindi.
Miongoni mwa miili hiyo ni ule uliookotwa Septemba 25, mwaka huu kwenye Ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam ukiwa na jiwe kubwa lililofungwa na kamba.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa jeshi hilo nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, ambaye pamoja na mambo mengine alizungumzia hali ya uhalifu nchini ambapo alisema matukio ya uhalifu yamepungua kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana.
Kuhusu miili hiyo kutopata watambuzi, IGP Sirro alisema licha ya jitihada zote ambazo zimeendelea kuchukuliwa na jeshi hilo, bado wananchi waliopotelewa na ndugu zao wamekuwa wazito kujitokeza kwa ajili ya utambuzi na hivyo kusababisha zoezi kuwa gumu.
Itakumbukwa Oktoba 5, mwaka huu IGP Sirro, alitoa wito kwa umma kwamba kama kuna mtu ambaye ndugu yake amepotea afike makao makuu ya jeshi hilo kitengo cha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ili kufanya uchunguzi kuona kama ni ndugu yake au la.
“Tulitangaza kuwa wale wote waliopotelewa na ndugu zao waje kwa ajili ya kuchukua vinasaba (DNA), lakini hadi leo (jana) bado hatujaona mtu yeyote, lakini pia bado tunaendelea na kufanya tathmini juu ya matukio hayo yaliyojitokeza hivyo bado uchunguzi wetu unaendelea,” alisema IGP Sirro.
Kuhusu matukio ya uhalifu wa kutumia silaha katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, alisema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata wahalifu ambao alisema wamekiri kufanya matukio mbalimbali ya mauaji huku baadhi yao wakikimbilia nchi za jirani.
“Tumeendelea kudhibiti uhalifu kwa kiasi kikubwa japo wachache bado wapo wakiwamo waliokimbilia kwenye nchi za Msumbiji na Congo DR na hivi karibuni tulipata taarifa walikuwa wameteka kijiji nchini Msumbiji, lakini kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi wahalifu hao wataendelea kushughulikiwa hata huko walikokimbilia,” alisema IGP Sirro.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi alisema nyumba za askari wa jeshi hilo zilizoteketea kwa moto kwenye maeneo ya Arusha zinatarajia kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi huu kwa kuwa tayari ujenzi wake umekamilika.
“Jumla ya nyumba 36 zinatarajiwa kukabidhiwa mwishoni mwa mwezi huu, ambapo jeshi limejenga unit 18 na 18 nyingine ni ushirikiano wa wafanyabishara wa mkoa huo, japo hiyo haina maana kuwa wakikutwa na makosa hawatashughulikiwa.
“Hivyo tunaomba wananchi wengine kujitolea kusaidia ujenzi wa nyumba za askari wetu kwenye maeneo mengine kama Geita, Mwanza na kwingineko,” alisema IGP Sirro.
No comments:
Post a Comment