Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akimkabidhi kadi ya bima ya afya, Irene Paul kwa niaba ya watoto wenzanke 139 ambao wanaishi katika mazingira magumu. Kadi hizo zimetolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na mfuko wa Abbott na benki ya ABC. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati wa benki ya ABC, Joyce Malai, Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Kurasini, Rabikira Mushi na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Miradi Endelevu wa Mfuko wa Abbott, Dkt. Festo Kayandabila na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali wa hospitali hiyo, Dkt. Juma Mfinanga.
Baadhi ya walezi wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakishuhudia jinsi watoto hao wanavyokabidhiwa kadi za bima ya afya leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili leo.
Waziri wa Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akizungumza kabla ya kukabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Baadhi ya watoto waliokabidhiwa kadi za bima ya afya na Waziri wa Afya wakionyesha kadi hizo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Muhimbili leo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza faida za watoto hao kupatiwa kadi hizo.
Baadhi ya wataalamu wa afya wa Muhimbili wakiwa kwenye mkutano huo leo.
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya ABC wakishuhudia shughuli ya kukabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto hao leo
……………
Serikali ameipa siku 60 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuandaa mpango utakaowawezesha wateja wa hiari kulipia fedha kidogo kidogo kwa ajili ya kupata kadi ya bima ya afya.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kabla ya kukabidhi kadi za bima ya afya kwa watoto 139 wanaoishi katika mazingira magumu. Kazi hizo zimetolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Mfuko wa Abbott na Benki ABC.
Waziri Ummy Mwalimu ameuagiza mfuko wa NHIF kuhakikisha ndani ya siku 60 inaweka utaratibu ambao utasaidia wateja wa hiari wanapata kadi za bima ya afya ndani ya muda mfupi kwa kuwa wengi wao hawana fedha taslimu Sh 50,400 za kulipia kwa wakati mmoja.
“Natoa siku 60 kwa NHIF kuhakikisha inaweka utaratibu wa kuwawezesha watu kupata kadi ya bima ya afya kwa kulipa fedha kidogo, kidogo kwa mfano mteja wa hiari anaweza kulipia Sh 5,000 au Sh 10,000 hadi atakapokuwa amefikisha Sh50,400 ambayo inatakiwa na NHIF,” alisema waziri huyo.
Katika hatua nyingine, serikali imeipongeza Muhimbili kutokana na juhudi za kuwawezesha wananchi kupata huduma bora ikiwamo kuwapatia kadi za bima ya afya watoto 139 wanaoishi katika mazingira magumu.Waziri huyo amesema uamuzi wa Muhimbili kutoa kadi kwa watoto hao ni mfano wa kuigwa na kwamba unapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini.
“Naamini mpango huu, utawaamsha wazazi, walezi na wadau wengine wa afya ili kuhakikisha kwamba watoto wa Taifa hili wanakuwa na bima za Afya mara tu baada ya kuzaliwa,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema Muhimbili kwa kushirikiana mfuko wa Abbot na Benki ABC imewezesha watoto hao kupata kadi ya bima ya afya ili waweze kupata matibabu popote pale watakapokwenda nchini.“Muhimbili imekuwa ikitekeleza jukumu lake kikamilifu la kutoa huduma bure kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kuchangia huduma kwa kiasi Sh milioni 500 hadi 600 kwa mwezi sawa na Sh. bilioni 6 hadi 7.2 kwa mwaka,” amesema Profesa Museru.
Profesa Museru amesema kadi hizo zitapunguza mzigo mzito kwa vituo vya kutunzia watoto ambavyo vimekuwa vikigharamia huduma za Afya kwa kutumia fedha taslimu pale watoto hao wanapougua.
“Mheshimiwa Waziri, nitoe rai kwa wenzetu NHIF kuangalia namna ambavyo huduma kwa kundi hili la watoto itaendelea kuwafikiaw ahitaji wengi ili kuhakikisha watoto wetu wanakuwa na uhakika wa kuzifikia huduma za afya popote pale,” amesema mkurugenzi huyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Juma Mfinanga amesema kutokana na uboreshaji uliofanywa na idara hiyo hivi sasa wanapokea wastani wa wagonjwa mahututi wapatao 200 hadi 250 kwa siku na kuwapatia huduma ya afya.
“Utafiti uliofanyika Muhimbili na kuchapishwa katika majarida mbalimbali ya kimataifa unaonyesha kuwa idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali imepunguza vifo MNH kwa zaidi ya asilimia 5 kutoka asilimia 13 kabla ya kuanzishwa kwa idara hiyo hadi asilimia 8 baada kunzishwa,” amesema Dkt Juma.
No comments:
Post a Comment