Saturday, November 25

Upasuaji wa Kihistoria Kupandikiza Figo Wafanyika Muhimbili


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upasuaji wa kihistoria wa kupandikiza figo ambao umefanyika Novemba 21, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa ni mara ya kwanza upasuaji huo kufanyika nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Profesa Lawrence Museru, Dkt. Rajesh Pande, Dkt Sunil na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya figo Muhimbili, Dkt. Jacqueline Shoo wakiwa kwenye mkutano huo leo.
Wataalamu wa figo wa Muhimbili ambao wameshiriki katika upasuaji huo wa kihistoria wakiwa kwenye mkutano huo leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, Dkt. Rajesh Pande na Dkt Sunil wakifuatilia mkutano huo.

Baadhi ya wataalamu wa magonjwa ya figo kutoka India wakiwa kwenye mkutano huo leo
Baadhi ya wafanyakazi wa Muhimbili na wataalamu wakifuatilia mkutano huo.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa afya na wafanyakazi wa hospitali hiyo. PICHA NA JOHN STEPHEN, HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI



Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya New Delhi, India imefanikiwa kufanya upasuaji wa kihistoria wa kupandikiza figo (Renal Transplant) ikiwa ni mara ya kwanza nchini.

Upandikizaji wa figo umefanywa na madaktari bingwa wa Mhimbili na Hospitali ya BLK Novemba 21, mwaka huu na taarifa za wataalamu hao zimeeleza upasuaji huo umekuwa wa mafanikio makubwa na kwamba utakuwa endelevu.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kufanyika kwa upasuaji huo ni moja ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuboresha na kuanzisha huduma bora za kibingwa nchini.

“Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha huduma za afya nchini chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli zikiwamo za kibingwa nchini na kupunguza rufaa za wagonjwa wanaohitaji huduma hizo nje ya nchi,” amesema Ummy Mwalimu.

Amesema upasuaji figo katika Hospitali ya Muhimbili utasaidia kupunguza gharama kubwa ambazo serikali imekuwa ikitumia kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

Waziri huyo amesema hivi sasa kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa figo na kwamba takwimu zinaonesha Muhimbili kuna wagonjwa 200 wanaofanyiwa huduma ya utakasishaji damu.

Amesema kutokana na ongezeko hilo, Serikali imeanzisha vituo vya utakasishaji damu katika hospitali za Mbeya Rufaa, Benjamin Mkapa, KCMC, Bugando na hospitali binafsi zikiwamo Kairuki, TMJ, Regency na Hindu Mandal.

“Kwa namna ya pekee nawashukuru wataalamu 11 ambao tupo nao hapa wakiongozwa na Profesa. H.S. Batyal, Dkt. Sunil Prakash, Dkt. Rajesh Kumar Pande na Dkt. Anil Handoo ambao kwa kushirikiana na wataalamu wetu wamefanikisha upasuaji huu. Pia, napenda kuwashukuru wakurugenzi, wataalamu pamoja na Wafanyakazi wote wa Muhimbili wakiongozwa na Prof. Lawrence Museru,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema kuwa mpango wa kupandikiza figo umewezeshwa na hospitali hiyo ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya kuboresha huduma za afya nchini.

Profesa Museru amesema awali ilipeleka India wataalamu kwa ajili ya kupata mafunzo ya kutekeleza mradi huo na kwamba umekuwa wa mafanikio makubwa nchini Tanzania.

Mkurugenzi huyo amesema mpango huo utasaidia kupunguza gharama kwa wagonjwa waliokuwa wanapelekewa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya figo.

Profesa Museru amesema upandikizaji wa figo ambao unajumuisha kumuandaa mgonjwa, vipimo mbalimbali vinavyohitajika kwa mpokeaji na mtoaji figo unagharimu wastani wa Sh. 21 milioni za kitanzania katika hospitali hiyo ya Muhimbili.

“Hii ni nafuu sana ukilinganisha na gharama ya Sh.80 hadi 100 milioni iliyokuwa ikitumiwa na Serikali kupeleka mgonjwa mmoja nje kwa huduma hii ikiwamo matibabu, usafiri na malazi. Hivyo basi, licha ya huduma hii kusaidia kuleta huduma za kisasa nchini pia, itakuwa ni nafuu sana na kuwezesha wagonjwa wengi zaidi kupatiwa huduma hiyo,”amesema Profesa Museru.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa mafanikio ya upasuaji huo utasaidia kuweka msingi wa kuanzisha programu nyingine za upandikizaji viungo (organ transplant) hapa nchini kama vile upandikizaji wa ini (liver transplant).

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wataalamu kutoka Hospitali ya BLK New Delhi, India ambao wameshirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa zaidi ya mwaka mmoja katika mipango na maandalizi ya utoaji wa huduma ya upandikizaji figo. Kwa namna ya pekee nawashukuru hawa wataalamu 11 ambao tupo nao hapa wakiongozwa na Profesa H.S. Batyal, Dkt. Sunil Prakash, Dkt. Rajesh Kumar Pande na Dkt. Anil Handoo ambao kwa kushirikiana na wataalamu wetu wamefanikisha upasuaji huu,” amesema Profesa Museru.

No comments:

Post a Comment