Friday, November 24

Wapiga kura wahakikishiwa usalama wao


Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema  uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Saranga iliyopo Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam utafanyika  Novemba 26,kama ilivyopangwa, licha ya kuteketea kwa moto vifaa vingi vya uchaguzi baada ya jengo la Ofisi ya Kata hiyo kuungua usiku wa kuamkia jana.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC) Hamis Mkunga  amesema hayo leo Novemba 24  baada ya kutembelea eneo la tukio na kueleza kuwa tayari ofisi yake imekwishafanya taratibu nyingine ili kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vilivyoteketea kwa moto vinapatikana na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.
“Tumefika hapa baada ya kupata taarifa za kuungua kwa jengo la Ofisi ya Kata ya Saranga ambalo pia tulihifadhi vifaa vya uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika  Jumapili  na bahati mbaya vifaa vingi vya uchaguzi vimeteketea vikiwemo  fulana na fomu mbalimbali’’ amesema
Ameongeza kwamba ‘’ Hata hivyo tayari tumefanya utaratibu wa kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana na uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa awali ”  amesema Mkunga
Aidha ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni hujuma kwani mashuhuda walipofika eneo la tukio walikuta dumu la mafuta ya petroli lakini hawajabaini sababu ya kutokea kwa hujuma hiyo na kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi zaidi.
Kuhusu hali ya usalama wakati wa uchaguzi Mkunga amesema  kuwa tayari vyombo vya usalama Wilaya ya Ubungo vimejulishwa na kuwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa usalama utaimarishwa na kuwataka wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.
Mkunga amesema  bado hawajaweza kubaini kiwango halisi cha hasara kilichopatikana na kutokana na ajali hiyo na kuwa ofisi yake inaendelea kufanya tathmini juu ya hasara hiyo.  
Naye Mkuu wa Idara ya Uchaguzi NEC,  Irene Kadushi  amesema kuwa, kata ya Saranga ina vituo vya kupigia kura 139 ambapo vifaa vyote vya uchaguzi awamu ya kwanza na ya pili vilikuwa vimekwishafika na kuwa awamu ya mwisho ya usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi katika kata hiyo ilikuwa ni jana asubuhi lakini wamelazimika kuzuia upelekaji wa vifaa hivyo kutokana na tatizo hilo.
Aidha amesema kuwa shughuli zote za uchaguzi ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uchaguzi zimehamishiwa katika Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa usalama zaidi, na kusisitiza kuwa taratibu nyingine zinaendelea na uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

No comments:

Post a Comment