Friday, November 24

Zabuni ya dawa Sadc fursa ya ujenzi wa viwanda


Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amesema hatua ya Tanzania kuteuliwa kuwa mnunuzi wa dawa wa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc) itatoa fursa mpya ya ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini.
Mkutano wa mawaziri wa afya na wanaohusika na masuala ya Ukimwi hivi karibuni ulipitisha uteuzi wa Tanzania kuwa mnunuzi wa dawa kwa nchi 15 wanachama wa Sadc.
Akizungumza na MCL Digital, leo Ijumaa Novemba 24,2017, Bwanakunu amesema faida ya kwanza kwa Tanzania kupata zabuni hiyo ni viwanda vya ndani kuwa na vigezo vya kuuza dawa Sadc.
Bwanakunu amesema hatua hiyo ni fursa mpya kwa Watanzania kuwekeza kwenye viwanda vya dawa na vifaa tiba kwa sababu ya uhakika wa soko.
“Watanzania wajipange kuuza vifaa tiba kama vile pamba, bandeji na hata maji ya dripu.  Tanzania haiwezi kuwa kituo halafu ishindwe kuwapa tenda wazabuni wanaokidhi vigezo wa hapa nyumbani,” amesema.
Bwanakunu amesema si lazima kuwekeza kwenye viwanda vya kitaalamu isipokuwa kwenye bidhaa za vifaa tiba jambo linalowezekana.
Mkurugenzi mkuu huyo amesema vifaa vingi vya tiba vimekuwa vikiagiwa nje ya nchi kutokana na kukosekana viwanda vinavyoweza kukidhi vigezo na kupewa tenda ya kutosheleza mahitaji hata yale ya ndani ya nchi.
“Niliwahi kutafuta kiwanda kwa ajili ya kununua peni za kusambaza kwenye vituo vya afya, hakuna ilibidi tuagize nje ya nchi. Kama kipo waje wanione tuwape biashara,” amesema.
Bwanakunu amesema hata maji ya dripu kwa sasa yananunuliwa nchini Uganda jambo alilosema ni la aibu kwa kuwa yangeweza kutengenezwa nchini.
Amesema nchi yoyote inayotaka kuendelea lazima iwe na viwanda na ni  jukumu la MSD na Serikali kufanya uwekezaji kwenye viwanda kwa vitendo.
Bwanakunu amesema MSD imetoa zabuni kwa viwanda vya ndani vilivyopo na zaidi ya Sh20 bilioni zimeshalipwa kwa wamiliki wake.
Amesema Tanzania ina viwanda vitano vya dawa vinavyofanya kazi na vingine vingi vinaanzishwa.
Amesema fedha inayozunguka kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa  ni zaidi ya Sh1.3 trilioni kwa maana ya ile ya Serikali, wafadhili, bima ya afya, wananchi na vyanzo vingine.
Akizungumzia namna MSD itakavyofanya kazi, Bwanakunu amesema itaweka kitengo maalumu ambacho kitakuwa kinashughulikia ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kupitia mfumo wa ununuzi shirikishi.
Bwanakunu alisema hatua hiyo itapunguza kwa kiasi kikubwa bei ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matumizi ya nchi wanachama wa Sadc.
Amesema watahakikisha wanatekeleza jukumu hilo kwa umakini na kwamba  wamejipanga kutangaza zabuni kwa nchi 15 kwa ajili ya kujua kiwango cha dawa ambazo zitakuwa zikipatikana kwa watakaoshinda zabuni hizo.

No comments:

Post a Comment