Monday, November 13

Wafanyakazi HESLB waaswa kuwa wabunifu

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiongea na menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Nov 13, 2017). Keshoto ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu Prof. Sylvia Temu na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru. (Picha na HESLB) 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Nov 13, 2017). Keshoto ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu Prof. Sylvia Temu. (Picha na HESLB) 
Baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Bodi ya Mikopo katika mkutano na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe ambaye amefanya ziara yake ya kikazi katika Ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Nov 13, 2017). (Picha na HESLB) 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe amewataka wafanyakazi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuongeza ubunifu ili kuondokana na changamoto wanazokutana nazo.

Prof. Mdoe amesema hayo leo (Jumatatu, Novemba 13, 2017) alipokua akiongea na Menejimenti ya HESLB katika ziara aliyoifanya katika makao makuu ya HESLB jijini Dar es Salaam.

“Pamoja na mafanikio mnayoyapata hasa katika ukusanyaji wa mikopo lakini bado kuna changamoto…zikiwemo za malalamiko ya vigezo vya utoaji mikopo ambavyo mnahitaji kuwa wabunifu kwa kuwashirikisha wadau,” amesema kiongozi huyo katika ziara yake ya kikazi.

Kwa mujibu wa Prof. Mdoe, nia ya Serikali ni kuona malalamiko yote ya wadau yanatafutiwa ufumbuzi kwa haraka, na ili hilo litimizwe ni muhimu kwa wafayakazi wa taasisi za umma kuwa wabunifu zaidi.

Awali akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu huyo katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul- Razaq Badru alisema taasisi yake imejipanga kuhakikisha huduma inazotoa zinaakisi matarajio ya Serikali na kwamba mkazo umewekwa kwenye kuongeza kasi ya ukusanyaji mikopo na kushirikisha wadau katika kuboresha vigezo vya utoaji mikopo kwa miaka ijayo.

“Katika mwaka 2016/2017 pekee, tulikusanya zaidi ya Tshs 116 bilioni na wastani wa makusanyo yetu kwa mwezi kwa sasa ni Tsh 12 bilioni. Tunataka kufikisha Tsh 15 bilioni kwa mwezi ifikapo mwakani,” amesema Bw. Badru katika mkutano huo uliohidhuriwa pia na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Sylvia Temu.

Wakati huohuo, HESLB imewakumbusha wanafunzi wote ambao hawajaridhika na mikopo waliyopangiwa au kukosa, kuhakikisha kuwa watatemebelea mtandao wa Bodi (olas.heslb.go.tz) wanakata rufaa na kuwasilisha kwa maafisa mikopo waliopo kwenye vyuo vyao kabla ya tarehe 19 Novemba mwaka huu.

Ufafanuzi huo unafuatia baadhi ya wanafunzi walikosa mikopo au kutoridhika na mikopo waliyopangiwa kufika katika ofisi za HESLB jijini Dar es Salaam na zile za kanda zilizopo Dodoma, Arusha, Mwanza na Zanzibar.

Mwishoni mwa wiki, HESLB ilitangaza kufungua dirisha la rufaa ambalo litafungwa Novemba 19, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili. Kwa muibu wa HESLB, lengo ni kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba 30, 2017.

Maelezo ya kina kuhusu utaratibu wa kuwasilisha rufaa yatatolewa kupitia tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz). 

No comments:

Post a Comment