Monday, November 13

TUME YA UCHAGUZI YAKUTANA NA VYAMA VYA SIASA KUELEKEA UCHAGUZI MDOGO

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa kwenye mkutano wa Tume na vyama hivyo ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Novemba 26, 2017. Mkutano huo umeliofanyika leo jijini Dar es Salaam leo.Kushoto ni Makamu Mwenyekiti Jaji  Mst. Hamid Mahmoud Hamid na kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani akitoa mada kwa viongozi wa vyama vya siasa wakati Tume ilipokutana na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam leo. 
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage (wa tatu kulia) akiwa meza kuu na Makamu Mwenyekiti Jaji Mst. Hamid Mahmoud Hamid( wa tatu kushoto), Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani )wa pili kulia), Makamishna wa NEC Jaji Mst. Marry Longway na Asina Omari na kulia ni Mwakilishi wa Mkuuu wa Jeshi la Polisi (IGP), kwenye mkutano wa Tume na vyama vya siasa uliofanyika Dar es Salaam jijini leo.
Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wakifuatilia hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage kwenye mkutano wa Tume na vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Yeremia Maganja akichangia mada kwenye mkutano wa Tume na vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani akizungumza na waandishi wa Habari baada ya ufunguzi wa mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo.
 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage   (kushoto) akisalimiana na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Pwani Casimir mabina.Katikati ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha UDP Saumu Rashid. 
Picha na Hussein Makame-NEC

Hussein Makame-NEC
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistolces Kaijage amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili ya Uchaguzi.

Jaji Kaijage ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa NEC na vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam leo kuelekea Uchaguzi mdogo wa madiniwa.

Alisema iwapo ukiukwaji au uvunjaji wa Maadili  hayo utatokea, Chama au Mgombea awasilishe malalamiko hayo mbele ya Kamati husika ili ishughulikiwe kisheria.

Aliwakumbusha kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 53 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 Tume inayo mamlaka ya kuruhusu kuwepo kwa Kampeni za Uchaguzi katika maeneo ya Uchaguzi na siyo Mikutano ya Vyama vya Siasa. 

Hivyo, kampeni hizo zifanyike kwenye Kata husika na inategemewa kuwa Mikutano ya Kampeni italenga kuwashawishi, kwa namna ya kistaarabu, wananchi wa Kata husika ili wamchague Mgombea anayefanyiwa kampeni. 

” Kwa mujibu wa kipengele cha 2.1. (c) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 tunategemea kila Chama cha Siasa kiendelee kufanya Kampeni kwa mujibu wa ratiba. Kampeni zote zinatakiwa kuanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni” alisema Jaji Kaijage. 

Aliongez kuwa kwa kuzingatia Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Tume imekwisha kutoa ushauri kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya ili katika kipindi hiki cha Uchaguzi wahakikishe wanazingatia wajibu wao na ukomo wa madaraka yao katika shughuli za Uchaguzi kuanzia kipindi cha Kampeni hadi kutangazwa kwa Matokeo. 

 Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi kailima Ramadhani aliaviomba Vyama vya Siasa kuwahimiza wanachama na wapenzi wao walioandikishwa kuwa Wapiga Kura wajitokeze  Siku ya Uchaguzi kwenda Kupiga Kura zao bila hofu yoyote  kuhusu usalama wao.

“Ni imani ya Tume kuwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mtakuwa chachu ya kuwaongoza na kuwaelekeza wanachama, wafuasi na mashabiki wenu katika kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu’ alisema Kailima.

Uchaguzi Mdogo wa madiwani katika kata 43 za Tanzania Bara, unatarajiwa kufanyika tarehe 26 Novemba, 2017 ambapo wapiga kura 333,309 wanategemewa kupiga kura siku ya uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment