Wakizungumza katika semina ya wabunge iliyoandaliwa na kampuni ya Maxcom Afrika leo Novemba 12, wamesema baadhi ya watumishi wa Serikali wamekuwa wakipiga vita kampuni zinazomilikiwa na wazawa.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema baadhi ya watumishi wameanza utamaduni wa kushusha ubora kazi zinazofanywa na wazalendo.
“Kuna kampuni moja ya kizalendo ilikuwa inahusika na E-migration (uhamiaji mtandao) imeendelea kwa miaka sita lakini wakubwa wanawanyang’anya na wanaleta watu wengine,” amesema
Amewataka watendaji kuacha wivu kwa wazawa wanapopata fursa za kukuza uchumi wa nchi.
Mbunge wa Ileje (CCM), Janet Mbene ameeeleza kusikitishwa na vita inayopigwa kwa kampuni ya Maxcom. Alisema baadhi ya idara za Serikali zimewanyang’anya baadhi ya huduma akiitaja Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Kama kuna sehemu wamekosea warekebishwe na si kunyang’anywa, adui lazima wawepo sasa tusirudi nyuma, tusiingize vitu binafsi kwenye masilahi ya Taifa, vitu hivi vinawakimbiza vijana nje,” amesema Mbene.
Mbunge wa Singida Magharibi, (CCM), Elibariki Kingu alisema inashangaza Serikali inawekeza fedha kuibua vipaji vya Watanzania lakini wakikua na kuanzisha kampuni baadhi ya watendaji wanawapiga vita.
“Acheni kuwavunja moyo wazawa na kuwawekea vikwazo, wasaidieni wakue zaidi Afrika Mashariki na kuna madai Serikali inawawekea vikwazo hata kuwalipa madeni yao,” amesema.
Akizungumzia mauzo ya hisa, Mtendaji Mkuu wa Zan Securities ambao ni washauri wa masuala ya hisa wa Maxcom, Raphael Masumbuko alisema kampuni hiyo inatarajia kuuza asilimia 25 ya hisa zake kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).
Amesema kwa sasa thamani ya kampuni hiyo ni Sh68 bilioni, hivyo baada ya mauzo ya hisa thamani itafikia Sh90 bilioni.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo ambayo ni ya kwanza kutoa huduma za ununuzi wa umeme wa Luku kwa njia ya mtandao, Jamson Kasati amesema kwa siku kampuni hiyo inapitisha miamala 600,000, huku uwezo wake kwa sasa ni kupitisha miamala milioni tano kwa siku.
Ahmed Lusasi ambaye ni ofisa mwandamizi wa Maxcom amesema kampuni hiyo inayotoa huduma pia Uganda, Msumbiji, Burundi, Rwanda na Zambia inatarajia kutoa huduma katika nchi 10 ifikapo mwaka 2020. Kodi inayolipa nchini ni Sh6.5 bilioni.
No comments:
Post a Comment