Sunday, November 12

Bodi ya Mikopo yatangaza orodha mpya ya mikopo


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha nyingine yenye wanafunzi 1,775 wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo.
Kwa orodha hiyo, jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasa imefikia 31,353.
Katika awamu ya kwanza, wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza walipangiwa mikopo; awamu ya pili (11,481) na ya tatu (7,901).
Taarifa ya HESLB iliyotolewa leo Jumapili Novemba 12,2017 na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, imesema orodha kamili ya wanafunzi hao inapatikana katika tovuti ya bodiwww.heslb.go.tz na pia imeshatumwa kwa vyuo husika ili kuwawezesha wanafunzi kufanya usajili na kuendelea na masomo.
“Tumekuwa tukifanyia kazi orodha za udahili ambazo tumekuwa tukipokea, na kila tunapokamilisha tunatoa orodha za wanafunzi waliopangiwa mikopo ambao wana sifa,” amesema Badru.
Badru katika taarifa kwa vyombo vya habari amesema Sh427.54 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2017/18 na tayari Serikali imeshatoa Sh147.06 bilioni kwa ajili ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2017/18.
Fedha hizo, Sh427.54 bilioni amesema ni kwa ajili ya wanafunzi 122,623 wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.
Wakati huohuo, HESLB imetangaza kufungua dirisha la rufaa kuanzia kesho Jumatatu Novemba 13,2017 hadi Novemba 19, 2017 ili kuwapa fursa waombaji ambao hawajaridhika na upangaji wa mikopo kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili. 
Badru amesema lengo la HESLB ni kuhakikisha wanatangaza orodha ya majina ya waombaji mikopo waliofanikiwa katika rufaa ifikapo au kabla ya Novemba 30,2017.
“Tunatoa wito kwa uongozi wa vyuo vyote kupokea maombi ya rufaa za wanafunzi na kuwasilisha kwa Bodi kabla ya Novemba 22,2017 ili kuiwezesha Bodi kutoa orodha ya waombaji waliofanikiwa katika rufaa zao ifikapo Novemba30, 2017,” amesema Badru.

No comments:

Post a Comment