Saturday, November 25

Vigogo CCM waibuka dakika za lala salama

Mgombea Udiwani wa Kata ya Nangwa Wilaya ya
Mgombea Udiwani wa Kata ya Nangwa Wilaya ya Hanang’, Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Portajia Baynit akiomba kura kwa wananchi wa kata hiyo katika kampeni ziliyofanyika Kijiji cha Nangwa hivi karibuni. Picha ya Maktaba 
Dar es Salaam. Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 nchini zinamalizika leo wananchi katika kata hizo kesho watawachagua madiwani wao baada ya kushuhudia mpambano mkali katika dakika za lala salama.
Tofauti na kampeni za miaka mingine ambapo vyama vya siasa vilikuwa vikichuana tangu Tume ya Uchaguzi (NEC) inapopuliza kipenga kuashiria kuanza kwa kampeni, safari hii hali imekuwa tofauti; Awali chama tawala kilionyesha kusuasua huku vyama vya upinzani vikiwekeza nguvu zaidi tangu mwanzo.
Tangu NEC ilipotangaza kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo mdogo viongozi wa juu wa vyama vya upinzani, hasa Chadema na ACT wamekuwa wakionekana katika majukwaa hayo huku CCM wakificha silaha zao.
Lakini mara baada ya mikutano juu ya CCM – Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu Taifa (NEC) iliyomalizika mwanzoni mwa wiki, vigogo wa chama hicho, bila shaka baada ya kupokea tathmini ya kampeni hizo, walianza kuonekana katika majukwaa wakiwanadi wagombea.
Hali hii imeongeza chachu kwenye kampeni hizo na kuamsha ushindani katika siku za mwisho.
Chadema ilivyotumia fursa
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho kwa zaidi ya wiki tatu mfulululizo walipita katika mikoa mbalimbali ambako uchaguzi wa marudio unafanyika.
Mbali na Mbowe, wengine waliokuwa katika misafara ya kampeni za chama hicho ni pamoja na Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na mambo ya Nje, John Mrema, wajumbe wa Kamati, Baraza Kuu pamoja na wabunge wa chama hicho.
Pengine chama hicho kiliona kiu ya wananchi ambayo walikosa mikutano ya kisiasa muda mrefu na kuonekana kutamani kusikia kinachoendelea kwenye ulingo wa siasa za mageuzi nchini, hivyo kuamua kuitumia fursa hiyo kikamilifu kwa kutuma viongozi wazito.
Hili lilijidhihirisha katika msafara wa kampeni za chama hicho kutokana na wananchi wengi kujitokeza kwenye mikutano hiyo na kusababisha misafara mirefu ya pikipiki, baiskeli na wengine kujipanga kandokando ya barabara wakiwalaki viongozi wa chama hicho.
Hata hivyo, hatua hiyo ilionyesha wazi kuwapa wakati mgumu polisi na kutumia mabomu ya machozi katika baadhi ya maeneo kama jijini Mwanza na Moshi kuwatawanya mashabiki waliojitokeza kuwalaki viongozi wa kuu wa chama hicho.
Mbowe aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema mikutano hiyo ya uchaguzi ina umuhimu mkubwa tofauti na ya hadhara huku mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alituma salamu kutokea Hospitali ya Nairobi, ambako anatibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma Septemba 7, akitaka wananchi kutumia nafasi hiyo kutoipigia kura CCM.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa chama hicho, John Mrema anasema kwa muda wa miaka miwili viongozi wa chama hicho walishindwa kuongea na wananchi hivyo chama kiliona ni fursa ya kipekee kuwafikia.
“Haikuwa mikutano tu ya kata pekee tulitumia mikutano hiyo kuzungumza na Taifa, tulitumia fursa vizuri ndiyo maana leo sasa kila mmoja anajua kinachoendelea.”
Anasema kuwa pia walitumia fursa hiyo kuwaleza wananchi ahadi ambazo ziliahidiwa na Rais John Magufuli, mfano ile ya Sh50 milioni kwa kila kijiji ili wajue Serikali yao imeshindwa kutekeleza ahadi zake.
Anaongeza kuwa kwa kuwatumia viongozi wake wakuu wamepata manufaa makubwa na wanaamini itachochea ushindi katika uchaguzi huo.
“Leo tunashuhudia hata wenzetu wamezinduka, wakati tunaanza waliona kama hili haliwahusu lakini sasa unasikia Lukuvi yupo mkoa huu na Kinana yupo Arusha,” anasema.
ACT-Wazalendo hawakuwa nyuma
Kama ilivyokuwa kwa Chadema, Kiongozi wa Chama hicho, Zitto Kabwe hakuwa nyuma, alitumia kampeni hizo kukinadi chama chake katika mikoa mbalimbali kuhakikisha anatoa fursa ya kuzungumza na wananchi kuhusu hoja mbalimbali za kitaifa.
CCM waibuka
Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa CCM ambayo katika kipindi chote ilionekana kutumia vigogo wake wachache tofauti na miaka iliyopita.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba na baadaye mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ndiyo walionekana katika wiki za kwanza za kampeni katika mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara.
Lakini tangu kumalizika kwa vikao vya uongozi vya chama hicho ambavyo pamoja na mambo mengine vilikuwa na jukumu la kufanya tathimini ya uchaguzi huo mdogo, vigogo kadhaa wa chama hicho walianza kuonekana wakiongeza nguvu katika maeneo mbalimbali.
Mara baada ya chama hicho kumsamehe aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba siku inayofuata alionekana katika kampeni akimnadi mgombea wa chama hicho jijini Dar es Salaam.
Si Simba pekee pia Katibu Mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana na Nape nao waliibukia katika majukwaa ya kampeni mkoani Arusha wakiongeza nguvu ili kuhakikisha chama chao kinapata ushindi.
Vilevile, kada maarufu na waziri wa zamani, Stephen Wasira na Mwenyekiti wa wazazi anayemaliza muda wake, Abdallah Bulembo pia waliibukia Mwanza.
Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema hatua ya chama hicho tawala kuamua kupeleka vigogo wao katika kampeni dakika za lala salama utakisaidia kukiongezea kura.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha, Profesa Gaudens Mpangala anasema kipindi cha kampeni ndiyo muda mzuri wa kutumia fursa ya kuzungumza ajenda za chama ili zieleweke kwa wapiga kura.
“Ni fursa nzuri. Wapinzani wameliona hili ndiyo maana wakaamua kutumia nafasi hiyo kupeleka hoja kwa wananchi ili kupinga yale yote yaliyokuwa yakiwaminya ili wananchi waamue.”
Profesa Mpangala anatoa mfano kuwa kwa muda wote wa miaka miwili hakukuwa na usawa katika shughuli za kisiasa nchini kutokana na chama tawala kutumia shughuli za kiserikali kufanya siasa huku upinzani ukikatazwa kufanya hivyo. Hawakuwa na njia nzuri kama wasingetumia nafasi hiyo walioipata katika kampeni.
Alisema mara kadhaa Rais akiwa katika ziara za kiserikali amekuwa akichomekea masuala mbalimbali ya kisiasa. Hakukuwa na usawa hata kidogo kwani walizuiwa kufanya siasa, hivyo fursa waliyoipata wameitumia vyema.
Hata hivyo, Profesa Mpangala anatahadharisha kuihusu mwenendo wa polisi wa kupiga mabomu ya machozi na kuwakamata wapinzani akisema ni kunanyima haki za msingi.
Anasema kipindi cha kampeni wanasiasa waachiwe wafanye kampeni za kistaarabu ili kuweka usawa badala ya kuwatisha kwa kuwakamata.
Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana anasema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa chaguzi za marudio kwa sehemu nyingi hazina mvuto sana na haziwezi kubadili upepo wa kisiasa nchini.
“Watu wanachagua mbunge au diwani katika kata moja, unawezaje kubadili matokeo ya kata zaidi ya 2,000 zilizokuwepo,” anasisitiza Dk Bana.

No comments:

Post a Comment