Saturday, November 25

Polisi wajipanga kulinda sherehe za kuapishwa Uhuru


Nairobi, Kenya. Jeshi la Polisi limeonya kuwa hakutakuwa na maridhiano yoyote juu ya usalama Jumanne ijayo siku ambayo Rais mteule Uhuru Kenyatta na makamu wake William Ruto watakula kiapo cha kuwatumikia Wakenya kwa muhula wa pili wa miaka mitano.
Tayari Kamanda wa polisi wa Nairobi, Japhet Koome amechora “ukanda mwekundu” ambao watu watazuiwa kuanzia saa 12:00 asubuhi. Maeneo ambayo kutakuwa na ulinzi mkali ni barabara za Mombasa, Uhuru, Museum Hill, Wangare Maathai, Thika na maeneo ya Aga Khan na eneo kuzunguka uwanja wa Kasarani.
"Hii ni siku ya kihistoria kwa nchi yetu...Hebu tuhakikishe inafanikiwa. Tunatarajia kutembelewa na wageni wengi wa kimataifa na wakuu wa nchi na serikali,” amesema Koome alipozungumza na wanahabari.
"Wageni watatua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta (JKIA) na kupita maeneo mbalimbali. Tunawataka wenye vyombo vya moto washirikiane ili kuwezesha misafara hii kufika kwa urahisi maeneo mbalimbali."
Aliongeza: "Mtu yeyote atakayethubutu kuanzisha fujo katika maeneo yaliyotajwa atashughulikiwa ipasavyo. Hakuna kitakachoathiri usalama wa wakuu wa nchi."
Miongoni mwa watu mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Uhuru ni Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Vilevile, wanatarajiwa wakuu wa nchi na marais kadhaa.

No comments:

Post a Comment