Akapewa lakabu Crocodile yaani mamba. Ni kawaida kwa viongozi wengi duniani kujipachika au kupewa lakabu zinazoshabihi matendo yao. Mathalan, aliyekuwa Rais wa Zambia hayati Michael Satta aliyeitwa King Cobra.
Wachambuzi wengi wa kisiasa waliamini kuwa Rais Mugabe alimfukuza kazi makamu wake ili mke wake Grace Mugabe achukue nafasi hiyo na hatimaye awe Rais wa Zimbabwe. Matokeo yake jeshi la nchi hiyo – wapiganaji walioshirikiana na Mugabe kumng’oa mkoloni, chama chake Zanu-PF, Umoja wa Vijana wa chama hicho na takriban wananchi wote wa Zimbabwe walicharuka kumtaka Mugabe ajiuzulu.
Mke wake, ambaye kwa wengi ndiye amekuwa chokochoko ya tukio hilo, amemkimbia mumewe na inadaiwa amekwenda Namibia. Grace alivuma kwa ulafi wa mali, ufedhuli na ubarakala. Miezi michache tu iliyopita alimpiga msichana na kumjeruhi vibaya kichwani kule Afrika Kusini alikokwenda kwa matanuzi. Mpaka sasa amekimbia kushtakiwa kwa kosa hilo.
Kwa kweli Mugabe amefanyiwa stahamala kubwa mno na watu wa Zimbabwe. Yangeweza kumkuta kama yale ya Haile Sellasie, aliyekuwa Rais wa Ethiopia; Tsar aliyekuwa kiongozi wa Urusi au Ceusesku na mkewe Helena aliyekuwa Rais wa Romania. Wote hao walidhalilishwa na kuhilikishwa kwa izara kubwa na viongozi waliochukua nafasi zao.
Itakumbukwa kwamba hayati Mwalimu Nyerere alimwomba Mugabe aachie ngazi kwa viongozi wengine baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mingi. Isitoshe, hata Rais wa zamani wa Zambia Keneth Kaunda, alimnasihi afanye hivyo lakini akakaidi.
Hakika la kujitakia halina majuto na wa kiranga haliliwi wala hawekewi matanga. Hatimaye Novemba 21, Mugabe alikubali kujiuzulu.
Wakati dunia ikisubiri nini kitajiri Zimbabwe baada ya kujiuzulu kwa Mugabe, yafaa kutafakari; hivi hii tabia ya viongozi duniani kote kufarakana na kuwafukuza, kuwaachisha kazi au hata kuwaua makamu au watu wao wa karibu kisiasa, inatokana na woga wa viongozi hao au usaliti wa wale wanaoshutumiwa na viongozi hao?
Mifano ipo mingi mno lakini hebu tuangalie Lin Piao kule China, Jenerali Ochoa kule Cuba, Diallo Telli wa Guinea, Chris Hani wa Afrika Kusini, Josiah Magama Tongogara wa Zimbabwe na Oscar Kambona wa Tanzania.
Lin Piao alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China wakati wa uongozi wa Mwenyekiti Mao Tse Tung. Ukiachia Mao mwenyewe, Lin Piao alikuwa na umaarufu mkubwa sawa au pengine zaidi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo wakati huo, Hayati Chou en Lai.
Watu wa China na nje ya nchi hiyo waliamini Lin Piao angekuwa mrithi wa Mao. Lakini ghafla, katika kile kilichoitwa mapinduzi ya kitamaduni yaliyolengwa kwa walioitwa ‘The Gang of Four’ yaani genge la watu wanne, Lin Piao alipotezwa mpaka leo. Hata picha zake alizopiga na Mao ziliondolewa. Imebaki kumbukumbu ya haiba, umbo jamali na bashasha yake tu, ambavyo ni silaha kwa wanasiasa wengi maarufu duniani.
Mwingine ni Jenerali Ochoa. Yasemekana huyu alikuwa miongoni mwa majemedari wachache waliotunukiwa nishani za juu za ushujaa nchini Cuba. Kwa Afrika, hususan Angola, Ochoa alitoa mchango mkubwa mno kuihami nchi hiyo dhidi ya majeshi ya uvamizi ya Afrika Kusini wakati wa uongozi wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo, Agostinho Neto.
Rais Neto alimwomba msaada wa kijeshi Rais Fidel Castro wa Cuba wakati wa uvamizi huo miaka michache tu baada ya uhuru wa nchi hiyo 1975. Kwa ustadi na ushupavu usiomithilika Jemedari Ochoa aliyaongoza majeshi ya nchi yake yaliyokuwa yakisaidiana na yale ya Angola kupambana na makaburu katika jiji la Quito Quanavalle! Vita hivyo vimebaki kuwa rejea ya ustadi mkubwa wa majeshi ya Cuba duniani.
Lakini baadaye, Fidel Castro akadai kuwa Jemadali Ochoa alikuwa anauza dawa za kulevya wakati akiwa Angola. Hatimaye alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi akapatikana na hatia. Dunia nzima ilimwomba Rais Castro asimpige risasi Jemadali Ochoa, lakini alikataa. Wengi waliingiwa na simanzi kubwa lakini ukawa mwisho wake.
Tukirejea Afrika tuanze na Diallo Telli wa Guinea ya Conakry. Huyu alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Kwa wanadiplomasia na wanasiasa wengi yeye ndiye aliweka misingi ya utendaji wa Umoja huo na kwamba aliwazidi wote waliomfuatia. Alizungumza Kiingereza na Kifaransa kwa ufasaha mkubwa. Aidha, kama vile Lin Piao wa China, alikuwa na mvuto na ucheshi mkubwa. Katika mazingira ya kutatanisha Diallo Telli alifungwa gerezani ambako inasemekana alinyimwa chakula kwa maelekezo ya Rais wa nchi hiyo, Ahmed Sekoui Toure. Akapewa maji tu mpaka mauti yakamkuta.
Wachambuzi wengi wa siasa na wanadiplomasia wanadai kuwa baada ya kukosa tena mvuto kwa raia wake alihofia Diallo Telli angechukua nafasi yake.
Tukimgeukia Chris Hani wa Afrika Kusini huyo alitoa mchango mkubwa kabisa katika ukombozi wa nchi hiyo. Wakati Madiba Nelson Mandela yuko gerezani na hata baada ya kufunguliwa, Chris Hani aliendelea kutoa mchango mkubwa wa ukombozi wa nchi hiyo. Miezi michache tu kabla ya uhuru wa nchi hiyo televisheni moja ya Uingereza iliendesha kipindi kilichoitwa Talking to Generals yaani Mazungumzo na majemadari ambapo Chris Hani alihojiwa yeye kwanza na baadaye Jenerali Daniel Otega wa Jeshi la Sandinista kule Nicaraguay ambako nako kulikuwa na harakati kama vile Afrika Kusini.
Kwa kifupi mabeberu, pamoja na makaburu wenyewe, walimuhofu zaidi Chris Hani kuliko Mandela. Yeye walimuona mithili ya Patrice Lumumba mwingine. Kwa hiyo kinadharia Hani alikuwa anahofiwa si na mabeberu tu bali pia na mabarakala waliotaka kutwaa uongozi wa nchi hiyo baada ya Mandela kuondoka.
Wako wanaoamini kuwa Thabo Mbeki na Jacob Zuma wasingethubutu kuwa marais wa nchi hiyo achilia mbali Cyril Ramaphosa ambaye dhahiri sasa anapigana kufa na kupona kuchukua nafasi ya Jacob Zuma licha ya kushtumiwa mno kutokana mauaji ya wafanyakazi wa kiwanda cha Platinum nchini humo miaka michache tu iliyopita.
Chris Hani alipigwa risasi na Kaburu mmoja siku chache tu kabla ya Uhuru wa nchi hiyo. Kitendo cha Kaburu huyo kutoa ushuhuda mbele ya Tume ya Ukweli na Upatanishi kiliamsha chuki zaidi kuliko upatanishi uliokusudiwa.
Naam, twende kwa Josiah Magama Tongogara wa Zimbabwe. Mkasa wake yeye unashabihiana na ule wa Chris Hani kwa kiasi fulani. Tongogara alikuwa kiongozi wa majeshi ya Zimbabwe dhidi ya akina Ian Smith na Serikali yao ya kikoloni wakati Mugabe anaongoza mapambano ya kisiasa hususan katika Mazungumzo ya Lancaster kule Uingereza yaliyoratibiwa na Serikali ya Uingereza kupata mustakabali wa uhuru wa Zimbabwe kati ya Ian Smith na wenzanke kwa upande mmoja na vyama vya upinzani kwa upande mwingine. Wakati huo Nyerere alikuwa ni mwenyekiti wa Nchi zilizo mstari wa mbele, ambazo ziliteuliwa na OAU kuratibu mazungumzo hayo.
Hivyo mara nyingi Robert Mugabe na akina Joshua Nkomo na Ndabaningi Sithole walikuja Dar es Salaam kutoa mrejesho wa maendeleo na kupata mustakabali maridhawa. Wakati mmoja mazungumzo yalisuasua na Ian Smith akatia nyodo ya kujitoa. Mwalimu akashauri kuwa njia nzuri ya kumrejesha Smith ni kumtia adabu ya kumpiga katika kitali, na kweli Tongogara aliifanya kazi hiyo vyema!
Siku chache kabla ya uhuru wa Zimbabwe, Tongogara alikufa katika ajali ya gari akitokea Msumbiji kurejea Zimbabwe. Haya, tumalize na Oscar Kambona.Ukimwacha Mwalimu Nyerere mwenyewe wengi wanaona hakuna waziri ambaye alikuwa na mvuto katika Baraza la Mawaziri wakati huo kama Kambona. Alikuwa na umbo jamali, mtanashati, mzungumzaji mzuri. Mtindo wake wa kupiga mpaka na kulaza nywele upande mmoja ulipata umaarufu na kuigwa na vijana wa wakati huo hasa wanafunzi. Pale wilayani Pangani alifungua bomba la maji katika kijiji ambacho hadi leo kilibatizwa jina la Kambona. Yeye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Tanu na kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara nyingi tu kama Tawala za Mikoa, Mambo ya Nje pia Ulinzi. Umaarufu wake uliongezeka wakati alipokuwa Waziri wa Ulinzi pale Jeshi lilipoasi mwaka 1963. Yumkini kuanzia hapo uhusiano wa Kambona na Mwalimu ulitetereka. Siku moja nilimuuliza kiongozi mashuhuri mno wa Tanu hadi CCM anieleze Mwalimu na Kambona waligombania nini? Akafikiri sana, kisha akanijibu taratibu, sijui! Akakaa kimya huku nikimkazia macho. Akahisi yaliyopita akilini mwangu, akajibu tena kwa mkazo, sijui.
Na kwa kweli hatujui tafrani kati ya marais au viongozi waliopo madarakani na makamu wao inaletwa na woga wao tu au usaliti wa kweli kama inavyodaiwa. Ila tuna hakika kabisa kuwa yaliyomkuta Rais Mugabe dhahiri yatawakuta viongozi wengine wote wa aina yake hususan Afrika.
Juzi tu Rais mpya wa Angola amemfukuza kazi Isabela Dos Santos binti wa Rais aliyetoka madarakani hivi karibuni Jose Dos Santos. Mwanamke huyo ambaye inasemekana Dos Santos alimzaa na Mrusi wakati akiwa mafunzoni nchini humo, aliwekwa katika wadhifa wa Mkuu wa Shirika la Petroli la Taifa na baba yake mwaka 2014. Ndani ya miaka michache tu amekua tajiri kupindukia. Ikumbukwe Angola ni moja ya nchi chache ambazo zimekuwa zikichimba na kuuza mafuta kwa miaka mingi kama Nigeria. Lakini vilema walioathirika wakati wa mapambano ya kudai Uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa wareno yaliyoongozwa na Rais wa kwanza wa nchi hiyo Agostinho Neto hawajafaidika kabisa na utajiri wa nchi hiyo. Angola ina wenye ulemavu wengi waliokatika miguu kutokana na mabomu ya kufukia ardhini yaliyotegwa wakati wa vita vya ukombozi.
Zamani, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Ghana, Dk Osagyefo Kwame Nkrumah alisema kuwa Afrika itakuja tawaliwa na wakoloni weusi.
Miongo kadhaa baadaye Profesa Kunde wa Cameroon aliunga mkono utabiri huo. Na mara kwa mara Mwalimu Nyerere alikuwa akisema, “Madikteta wengi ni wa kwetu,” dhahiri akiwalenga viongozi wa Afrika.
Afrika ina viongozi ambao wamekaa madarakani zaidi ya miaka ishirini na hawataki kuondoka kwa kudai eti wanaleta maendeleo nchini mwao na kupendwa na raia wao. Hao ni pamoja na Rais Kabila wa Congo Kinshansa, Yoweri Museni wa Uganda, Paul Bia wa Cameroon, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Paul Kagame wa Rwanda, Yumkini pamoja na kupendwa sana kulikuwa na majaribio mawili ya kutaka kuipindua Serikali ya Mwalimu Nyerere ambayo yaliisha kwenye kesi mbili maarufu za uhaini.
Ya kwanza ni ile ya Gray Likungu Mattaka na Wenzake ambayo ilimhusisha Bibi Titi Mohamed, aliyeshiriki kikamilifu katika harakati za uhuru wa Tanganyika. Ya pili ni ile ya Khatibu Ghandi kwa lakabu McGhee na wenzake. Na wala mambo hayataishia kwenye viongozi tu. Yatavikumba vyama vyote tawala vinavyokandamiza upinzani kwa madai ya kuleta maendeleo. Watu hawataridhika na kile kinachodaiwa kubadilisha awamu za urais tu ndani ya vyama hivyo. Leo takriban vyama tawala vyote vilivyoanzishwa kugombea uhuru wa nchi za Afrika vimekufa. Daima watu wataendelea kudai demokrasia ya kweli kwa manufaa na ustawi wa raia wote. Chambilecho Nabii Issa Bin Mariam, yaani Yesu Kristo, “ Maisha si mkate na siagi tu.”
No comments:
Post a Comment