Vigogo waliohamia CCM na kutangaza uamuzi wao katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha.
Wengine walitoka ACT – Wazalendo, ni aliyekuwa mshauri wa chama hicho (sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji), Profesa Kitila Mkumbo; aliyekuwa Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, Mshauri wa Sheria, Albert Msando na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Edna Sanga.
Siku hiyo pia, Rais Magufuli alitangaza kumsamehe kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Sophia Simba. Sophia alifukuzwa uanachama kwa madai ya kukisaliti katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Hatua hii ya vigogo hao kuhama vyama vyao imekuja wakati tukielekea katika uchaguzi mdogo wa madiwani kujaza nafasi 43 kwenye halmashauri tofauti 36 zilizobaki wazi kwa sababu mbalimbali. Wengi wanaona kuwa usajili huu mkubwa ni njia ya kuongezea nguvu kampeni ya CCM katika uchaguzi huu.
Wengine wanasema labda hiki ni kisasi cha CCM dhidi ya upinzani uliofanikiwa kumpata Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye pia alikuwa mbunge wa Singida Kaskazini aliyejiondoa kwenye chama hicho.
Vyama vijiulize
Ni rahisi sana kupuuza waliohama na kudai wana njaa, wana tamaa na kadhalika. Inawezekana kuwa ni kweli, lakini inawezekana hoja walizozitoa dhidi ya vyama vyao vya upinzani pia zina uzito wake na hazingefaa kupuuzwa.
Ufuatiliaji wangu katika uendeshaji wa vyama, nimegundua jambo moja, wanaohama CCM mara nyingi ni kwa sababu ya udhaifu wa sera na utekelezaji wa sera hizo; lakini kwa upande wa upinzani wengi wanaovihama vyama hivyo ni kwa sababu ya muundo na uendeshaji wenyewe wa vyama, usiotoa fursa kwa watu wapya kupenya nafasi za juu.
Kwa vyama vya upinzani, inaonekana kuna genge la wachache ambao ndio huamua kati yao nani ashike madaraka, badala ya kuachia demokrasia ifanye kazi. Mwaka 2015 na miaka yote ya kupokezana vijiti vya urais, ndani ya CCM kumekuwa na kinyang’anyiro cha kupigania tiketi ya urais kupitia mchakato mzuri na shirikishi katika vikao mbalimbali vya chama, hadi kufikia mkutano mkuu.
Watu huchujwa kwa vigezo vya kimaadili vinavyojulikana. Ni michakato kama hii ndiyo inayotoa fursa kwa akina Magufuli waliokuwa nje ya waliotarajiwa kupata madaraka.
Nimeandika sana hili na sitaacha kuliandika, kwamba, umefika wakati sasa vyama vya upinzani viboreshe demokrasia ya ndani ya vyama vyao, na waache kufikiria kuwa wachache miongoni mwao ndio wanaojua nani anafaa kuwa kiongozi mkuu.
Suala la ajenda pia ni la kuzingatiwa, kama ambavyo liliibuliwa na David Kafulila ambaye pia amehama Chadema. Yeye anaamini vyama vya upinzani vimehama katika ajenda ya kupambana na ufisadi. Mimi naamini ufisadi ungalipo, ila umebadilika sura yake tu.
Hivyo basi, vyama vya upinzani vinapaswa kuendelea na kupambana na ufisadi uliochukua sura mpya katika awamu hii.
Ufisadi mpya katika awamu ya tano unaweza kuuona katika ukiukwaji wa sheria na maadili ya kiuongozi kwa baadhi ya maofisa wa umma, kwa kisingizio cha maslahi ya umma, taifa na kadhalika pamoja na undumilakuwili (double standard) katika kuchukua hatua mbalimbali.
Kuhama haki ya kiraia lakini...
Kuhama chama, kimsingi, ni haki ya kiraia. Kama ambavyo, mtu ana haki ya kujiunga na chama, pia anayo haki ya kujitoa. Hakuna kulazimishana. Hata hivyo, chama kimoja kinapotumia faida ya kuwa madarakani na uwezo wa kifedha ‘kuhamasisha’ walio katika vyama vingine kuhama, hapo pana tatizo.
‘Uhamasishaji’ wa kumfanya mtu ahame unaweza kufanyika kwa namna mbili, uhamasishaji chanya na uhamasishaji hasi.
Uhamasishaji chanya ni kumhonga mtu ama kwa pesa au cheo. Mfano wake ni kama zile tuhuma zilizowahi kutolewa na chama kimoja cha upinzani, na kufikishwa Takukuru, kuwa madiwani wao walihongwa pesa au kuahidiwa ajira ili wajiuzulu nafasi zao. Uhamasishaji hasi ni pale chama kimoja kinapotumia vitisho dhidi ya ‘uwekezaji’ au ‘biashara’ ya mtu.
Kama hamahama hii inayoendelea inatokana na mapenzi yao, kwa hiari yao, bila ushawisho wa kihalifu au mbinyo wowote, hakuna tatizo. Lakini tukumbuke kuwa, kumekuwa na tuhuma za rushwa katika kuchochea wanasiasa kuhama vyama, huku wengine wakidhaniwa kuwa wametishwa na hali inavyoendelea. Kama ni kweli, basi uhamaji huu wa vigogo, unaweza kudhoofisha demokrasia na siasa za ushindani.
Hakuna ushahidi wa moja kwa moja uliothibitika katika mahakama unaoonyesha kuwa kulikuwa na uhongaji wa vigogo waliohama karibuni au wale madiwani waliojiuzulu, lakini ushahidi wa mazingira ya jumla ya siasa za Tanzania katika awamu hii unaweza kushawishi watu kuamini kuwa kuhama huku siyo kwa kutaka bali ni kukidhi maslahi binafsi.
Si siri kuwa wapinzani katika awamu ya tano wapo katika mazingira magumu. Licha ya vikwazo vingi katika ufanyaji siasa, wengi wamejikuta wakikamatwa na kufunguliwa mashtaka mbalimbali ya uchochezi na mengineyo. Kwa ujumla, mazingira si rafiki kwa siasa za upinzani.
Ni hoja yangu kuwa, kama Serikali inaona haja na umuhimu wa kuwa na siasa za ushindani, ni bora iangalie upya mazingira inayoyajenga ya ufanyaji siasa. Ama la, kama imeonekana, siasa za ushindani hazina umuhimu tena, tunaweza kuendelea katika hali hii na hakika upinzani utadhoofika na karibuni tunaweza wote tukawa CCM.
Kwa dhana ile ya kuwa waliohama walibinywa wakashindwa kuvumilia na hivyo kuamua kujisalimisha, kuna baadhi ya watu wanawalaumu hao waliohama na kujisalimisha kuwa ni wajinga na waoga.
Ninachoamini mimi ni kuwa, ikiwa Serikali inataka kweli kuua upinzani, inaweza kwa sababu ukweli ni kwamba kila chuma kina kiwango chake cha kuyeyuka, kadhalika sisi binadamu. Kuna mahali tukifikishwa, tunakubali yaishe.
Katika maisha, kuna mambo muhimu kuliko chama, kama familia kwa mfano. Kama kuna jambo unafanyiwa ambalo linaenda kuathiri familia yako, unawezaje kuitoa kafara eti ili tu kuthibitisha uzalendo wako kwa chama.
Hoja yangu ni kwamba, kama kuna mbinyo usio wa haki, tusiwalaumu waliohama vyama, bali chama tawala na Serikali yake. Uhai wa upinzani unategemea sana dhamira nzuri ya Serikali.
Wanasiasa vigeugeu
Kuhama chama ni haki ya mtu, lakini kuna gharama kubwa kwa hao wahamaji. Na hapa zaidi nazungumzia zaidi aina ya wahamaji sugu – kama Kafulila, Masha, Kitila n.k- ambao hutoka chama A, akaenda chama B kisha akarudi chama A.
Ukihama vyama kwa aina hii, kuna namna ambayo watu wanaweza kukutazama – kama vile mtu asiyeaminika, muongo, mnafiki, anayeangalia tumbo lake zaidi asiye na msimamo, anayeyumba, asiye tayari kupambana na changamoto bali huzikimbia.
Hata wale wahamaji wa mara moja akina Katambi na Msando nao wanatia shaka ukizingatia matamshi yao ya ukosoaji dhidi ya CCM, tena siyo ya zamani bali ukosoaji dhidi ya Serikali ya awamu hii ya sasa. Katika muktadha mpana uhamaji huu wa wanasiasa kutoka chama kimoja hadi kingine, unatupa picha juu ya ‘tasnia’ ya siasa na hali ya wanasiasa.
Wanasiasa wetu, wanaweza kukwambia jambo moja asubuhi lakini mchana akatoa lugha tofauti kabisa. Hali hii inakufanya ujiulize, wanaposimama majukwaani wanamaanisha wanachokisema au tuwazingatie kama wana tasnia wenzao- wa Bongo Movie,
No comments:
Post a Comment