Thursday, November 9

USAFIRI: Daladala jijini Dar es Salaam kuanza kutumia kadi maalum za malipo


Dar es Salaam. Daladala jijini hapa zitaanza kutumia kadi maalumu za malipo ili kuondokana na changamoto za kulipa kwa fedha taslim.
Matumizi hayo yanayoanza leo yanatokana na uzinduzi wa kadi hizo uliofanyika jana.
Kadi mpya aina ya ‘Uhuru Pay’ zimeanza kufanya kazi katika baadhi ya daladala ikiwa ni hatua ya majaribio na zimezinduliwa na kampuni ya BCX ya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa BCX-Tanzania Seronga Wangwe alisema lengo la kubuni mfumo huo ni kutaka kuboresha ukusanyaji wa mapato ya vyombo hivyo na kuwapa uhuru watumiaji wa daladala kusafiri kwa utulivu.
“Tunataka kuondoa vurugu za kukosa chenchi na wizi unaofanywa kwenye daladala badala yake pesa iende moja kwa moja katika akaunti benki. Abiria na kondakta wasilazimike kuwa na fedha taslimu,” alisema.
Licha ya abiria na makondakta, alisema tofauti na ilivyokuwa awali hivi sasa wamiliki wa vyombo hivyo wataweza kupata faida katika uwekezaji wanaoufanya kutokana na udhibiti wa mapato ya makusanyo.
Alisema katika hatua za awali mfumo huo umeanza kujaribiwa katika mabasi kumi yanayofanya safari zake kati ya Tegeta Nyuki na Kivukoni kabla ya kuhamia katika maeneo mengine ya jiji.
“Tunataka kubaini changamoto zilizopo kabla ya kufanya maboresho kukidhi mahitaji ya watumiaji na mifumo yetu ina uwezo wa kuhudumia watu wengi bila kuzidiwa tofauti na mingine,” alisema
Mfumo huo utaunganishwa moja kwa moja na wamiliki wa mabasi ili waweze kufuatilia mauzo ya tiketi ya kila siku kitu walichokosa kwa muda mrefu kwenye biashara hiyo.
Meneja wa usalama barabarani na mazingira kutoka Mamlaka ya Usafiri Majini na Nchikavu (Sumatra), Godfrey Silanda alisema wamefanya marekebisho ya kanuni kuendana na mfumo huo.
“Kwa mujibu wa TBS, watu nane wanaruhusiwa kusimama katika mita moja ya mraba. Lakini kwa kuzingatia aina ya basi, kila moja litakuwa na utaratibu wake,” alisema Silanda.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya Christiania, Emmanuel Mlaponi alisema mfumo huo utasaidia kuongeza mapato kwa kupunguza wiziunaofanywa na madereva au makondakta wasio waaminifu.
“Ilikuwa ni taabu kufutilia mapato. iNililazimika kuwafuata hawa wenzetu na nikawaambia wafikirie ni jinsi gani wanaweza kuniondolea changamoto hii.  NKuanzia sasa fedha itakua haipiti katika mikono ya mtu na itaenda benki moja kwa moja,” alisema Mlaponi.

No comments:

Post a Comment