Akifungua kikao kazi cha mawaziri kilichofanyika juzi katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma, Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao wakajiridhisha kwanza kama jambo wanalotaka kulitolea tamko halitakuwa na athari za kibajeti na kisera na kujiridhisha kama lipo katika bajeti za wizara zao.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri baada ya kikao hicho imesema Majaliwa pia amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.
“Tunao wajibu wa kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Magufuli na wananchi wote kwa jumla,” alisema.
Majaliwa, ambaye alikuwa naibu waziri wa Tamiseni na ambaye ni mtendaji mkuu wa Serikali, aliwataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, utaratibu na kanuni.
Ndoa kwa cheti cha kuzaliwa
Ingawa Waziri Mkuu hakuwataja viongozi hao, mawaziri wamekuwa wakitoa maagizo tofauti, yanayoonekana kukinzana na sera na pia kutozingatia uwezo wa kibajeti.
Mapema mwaka huu, Dk Harrison Mwakyembe, akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, alikaririwa akisema mwananchi ambaye hatakuwa na cheti cha kuzaliwa, hataruhusiwa kufunga ndoa.
Dk Mwakyembe alipiga marufuku watu kufunga ndoa ya aina yeyote, iwe ya Serikali, kimila au ya dini bila kuwa na cheti cha kuzaliwa, agizo ambalo alitaka lianze Mei Mosi.
Lakini nsiku moja baadaye, Rais John Magufuli alifuta agizo hilo akisema halitekelezeki.
“Dk Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu masharti hayo kutumika, kwa kuwa yatawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji,” inasema taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa.
Pia, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba aliwahi kuagiza kuwe na mizani maeneo yote ambako nyama inauzwa, zikiwemo sehemu za nyama choma ili wateja wanufaike na viwango halisi badala ya kukadiriwa. Hata hivyo, agizo hilo la mwaka 2016 wakati Kilimo kikiwa pamnoja na mifugop na uvuvi, halijatekelezwa,
Waziri mwingine ni Selemani Said Jafo wa Tamisemi ambaye aliagiza halmashauri 12 kuwa zimelipa madeni yake Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ifikapo Desemba 30.
Waziri mwingine anayedaiwa kutoa kauli zenye utata ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda ambaye aliwataka viongozi wa dini nchini kujihadhari kuwaozesha wasichana ambao hawajamaliza kidato cha nne.
Alisema watoto wa kike wanashindwa kumaliza masomo kwa sababu ya mimba au kuozeshwa jambo ambalo limeendelea kuisumbua Serikali katika juhudi zake za kuokoa maisha ya watoto wa kike ili waendelee na masomo.
“Haiwezekani mtu anamkamata mtuhumiwa anatakatisha Sh1 milioni anakosa dhamana, halafu mtu anampa mimba mwanafunzi kisha anapata dhamana siku hiyohiyo, hapa tutakuwa hatuthamini maisha ya mtoto wa kike.”
“Tunapoelekea watoto wote watasoma shule kuanzia darasa la kwanza mpaka form four, sera yetu mpya ambayo tutai –adopt hivi karibuni inasema mwaka mmoja wa shule ya awali, miaka sita shule ya msingi na miaka minne ya sekondari ni lazima. Kwa hiyo tunapoelekea, ili mtoto aolewe lazima aonyeshe cheti cha kumaliza shule ya sekondari... Ndiyo... ili uolewe uonyeshe living certificate au vinginevyo tujue wewe hujasoma kabisa ili tuwahoji wazazi..”
Hata hivyo, siku moja baada ya kauli hiyo ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii, Serikali ilikanusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ( Tamisemi ), Selemani Jafo alisema habari hizo kuwa msichana atatakiwa kuwa na cheti cha kidato cha nne kabla ya kuruhusiwa kufunga ndoa ni za upotoshaji.
Kufuatilia utekelezaji
Waziri Mkuu pia amewataka mawaziri kufuatiliaji na kutathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Alisema mawaziri na manaibu wao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21 na utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na ahadi alizotoa Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Wasomi, wabunge wapongeza
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu agizo hilo la Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema hatua hiyo itawarejesha katika mstari mawaziri ambao walikuwa wanatoa matamko yasiyotekelezeka.
Alisema Waziri Mkuu ni kiongozi wa mawaziri hivyo ni vizuri kuwarudisha katika mstari ili kuhakikisha hawatoi matamko yatakayoiweka Serikali njia panda.
“Kuna waziri aliwahi kusema ili kuolewa ni lazima mtoto amalize kidato cha nne, hivi wasiofika ndiyo wasiolewe?” alihoji.
“Wengine wanasema watafanya mambo makubwa ya maendeleo ilhali wanajua kabisa hayatekelezeki, ni vizuri kusema kitu unachokiamini na unachoweza kukifanya.”
Mwingine aliyempongeza ni Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye alisema Waziri Mkuu amekuwa mwerevu hasa kipindi hiki cha vyama vingi ambacho Serikali inafanya kazi na upinzani kama paka na panya.
“Unapokuwa serikalini wewe ni panya na upinzani ni paka, hivyo mara zote kuwindana ni jambo la kawaida cha msingi ni kuwa makini na matamshi yako,” alisema.
Alisema kwa sasa mawaziri wengi ni wageni hivyo Waziri Mkuu akiwa kiongozi wao ni lazima ahakikishe anasimamia wanasema nini, wakati gani na yataleta madhara gani kwa jamii.”
Alitoa mfano wa kauli iliyotolewa bungeni hivi karibuni na waziri mmoja kwamba hata vyerehani vinne ni kiwanda, akisema haikupaswa kutolewa na waziri.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Peter Msigwa alisema agizo hilo ni zuri lakini ni gumu kulitekeleza.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Oscar Mkasa alisema hiyo ni kanuni ya kawaida ya utawala ya Serikali kufanya uratibu katika shughuli zake.
“Ni agizo zuri kwa sababu wananchi watahoji matamko yaliyotolewa na Serikali hivyo ni namna nzuri ya kuratibu,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Kunti Majala alisema kutoa matamko ambayo hayatekelezeki ni mfumo ulioanza tangu zamani.
No comments:
Post a Comment