Jaji mmoja wa ngazi ya juu Uhispania amesema mahakama za nchi hiyo zinaweza kutoa waranti ya Ulaya ya kukamatwa kwa rais wa zamani wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont, baada ya kushindwa kufika mahakamani.
Mwanasheria wa kiongozi huyo kutoka Ubelgiji, ambako alisafiri pamoja na wanachama wanne wa baraza lake lililofutwa, amesema mazingira nchini Uhispania hayakuwa "mazuri" na mteja wake anataka "kujiweka mbali" lakini yuko tayari kutoa ushirikiano kwa mahakama. Paul Bekaert ameliambia shirika la habari la reuters kuwa mteja wake yuko tayari kutoa ushirikiano kwa mahakama za Uhispania na Ubelgiji zikimtaka afanye hivyo.
Puigdemont ambaye jana Jumatano alisema kwamba asingetii amri ya mahakama ya kurejea Uhispania ili kujibu mashitaka ya uasi na matumizi mabaya ya fedha yanayohusiana na jitihada za jimbo hilo kutaka kujitenga, hakutokea leo katika mahakama ya juu. Kufuatia hali hiyo rais wa mahakama ya juu Carlos Lesmes ambaye pia ni mkuu wa baraza kuu la mahakama ambalo ni chombo cha juu cha mahakama ametoa kauli inayoashiria kutolewa kwa waranti.
"Mtu asipotokea baada ya kuitwa na jaji kwa ajili ya kutoa ushahidi nchini Uhispania au katika nchi yoyote Umoja wa Ulaya, kawaida waranti ya kukamatwa inatolewa," amesema Carlos.
Ikiwa waranti ya kukamatwa itatolewa itamuwia vigumu Puigdemont kushiriki uchaguzi wa mapema katika mkoa huo tajairi ulioitishwa na serikali ya Uhispania hapo Desemba 21. Waendesha mashitaka wa Uhispania wanataka maafisa kadhaa wa zamani wa jimbo hilo kuwekwa kizuizini kabla ya kesi na kunyimwa dhamana. Jaji anayesikiliza kesi hiyo Carmen Lamela anapaswa kuamua ikiwa atakubaliana na ombi la waendesha mashitaka.
Wabunge wengine watano wa jimbo hilo na spika wa bunge la Catalonia Carme Fercadell ni miongoni mwa walioitwa na mahakama ya juu ambayo inahusika na kesi za watu walio na kinga ya bunge.
Mahakama ya juu imekubali leo kutoa wiki moja zaidi kwa Forcadell na wabunge wa Catalonia kwa ajili ya kujiandaa na utetezi na kesi hiyo itasikilizwa tena Novemba 9. Hadi kufikia saa tano asubuhi, wanachama watano wa baraza la Catalonia lililofutwa tayari walikuwa wametoa ushahidi wao mbele ya jaji wa mahakama kuu, ambaye ataamua ikiwa ataanzisha uchunguzi wa kina unaoweza kuchukua miaka kadhaa na kusababisha kesi.
Wakati hayo yakijiri, maelfu ya raia walikusanyika nje ya makazi ya rais wa Catalonia mjini Barcelona, wakionyesha kuwauunga mkono maafisa walioitwa mahakamani mjini Madrid. Umati huo wa watu ulikuwa ukipiga mokofi na kuimba nyimbo za uhuru wakibeba pia bendera za Catalonia.
No comments:
Post a Comment