Kisumu, Kenya. Katika maeneo mengi ya Nyanza nchini Kenya ambako maelfu ya watu wamekuwa wakijitokeza katika harakati mbalimbali wakiunga mkono muungano wa Nasa, Raila Odinga ndilo jina lililo vinywani mwa wengi.
Watu wengi wamekuwa wakijitokeza barabara kuandamana na hata kabla ya uchaguzi wa marudio uliofanyika siku chache zilizopita uliompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta, maandamano lilikuwa ni jambo la kawaida.
“Yeye ni masia wetu,” anasema Gordon Ochieng akiwa amekaa nyuma ya kanisa katika maeneo ya watu wenye uwezo mdogo la Nyalenda huko Kisumu.
Marudio ya uchaguzi
Wakati wa uchaguzi wa marudio Jiji la Kisumu lilikuwa na jukumu moja – kuandamana. Maandamano yaliyofanyika yalikuwa ya kupinga uchaguzi wa rais ulioitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) baada ya Mahakama ya juu kufuta matokeo ya urais ya Agosti 8 yaliyompa ushindi Kenyatta.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita wakazi wa Kisumu na maeneo ya jirani wamekuwa na harakati za maandamano ama kupinga mipango ya IEBC au kauli mbalimbali zilizotolewa na upande wa Jubilee, na mara zote maandamano hayo yalilenga kumuunga mkono Odinga.
“Hapa neno lolote la (Raila) Odinga inaweza kuwa sheria,” anasema mchungaji Francis Omondi.
Ingawa ushawishi wake wa kisiasa sio kama aliokuwa nao miaka iliyopita, juhudi zake pia za miaka 20 kuwa rais zinaendelea kukumbana na vipingamizi.
Ukoo wake umeshindwa kuinasa nafasi hiyo tangu Kenya ilipopata uhuru mwaka 1964.
Kisumu ni ‘yake’
Kutoka mitaa hadi katika majina ya hospitali, jiji lote linaonekana limehanikizwa na ‘nasaba’ ya Odinga ambayo ilianzishwa na baba yake, Jaramogi Oginga Odinga aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Kenya kabla ya kuongoza upinzani kwa muda mfupi, lakini kamwe hakuitawala Kenya.
Akijulikana kama “baba”, Odinga (mtoto) alizaliwa katika mji wa Maseno uliopo karibu na Kisumu ambao ni mkubwa katika eneo la mwambao wa Ziwa Viktoria.
Familia yake inamiliki mali nyingi ikiwa na makazi kwenye kilima kinachotazamana na ziwa hilo.
Wakati wa uchaguzi wa Agosti 8 ambao ulibatilishwa na Mahakama ya Juu katika hatua ambayo ilisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya, zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Kisumu na maeneo ya jirani walimpigia kura.
Na wakati mwanasiasa huyo alipowataka wafuasi wake kususia uchaguzi wa Oktoba 26, eneo lote la magharibi mwa Kenya lilifanya hivyo na ilikuwa nadra kuwaona watu wakiwa wamekaa.
‘Hatukupiga kura’
Siku ya uchaguzi wa marudio kaunti nne za magharibi mwa Kenya hazikupiga kura kabisa na IEBC ilitangaza kuuahirisha katika maeneo hayo hadi itakapotangaza upya siku ya uchaguzi.
Hali hiyo ilitokana na wafanyakazi wa IEBC kushindwa kujitokeza kusimamia kazi hiyo wakihofia kufanyiwa vurugu na waandamanaji waliotawala katika viunga vya jiji hilo.
Inaelezwa kwamba katika baadhi ya maeneo waandamanaji walifunga vituo vya kupigia kura kwa makufuli na sehemu zingine kuchomelea kwa umeme mageti ili kuwazuia wasiingie.
Wakati ushindi wa Kenyatta ulipokuwa ukingoni kutangazwa kulikuwa na hisia kwa mbali kutoka kwa wakazi wa Kisumu na maeneo jirani.
“Hatujali kwamba (Kenyatta) amekuwa rais, sisi hatujali maana hatukumchagua,” anasema Alex Onyango (24) anayefanya kazi katika bustani huku akitingisha mabega kuashiria kwamba ushindi wa Jubilee haukuwa lolote.
“Rais wetu ni ‘baba’,” anasema Robert Okello (28). Wengi wa wananchi wa kabila la Luo wanahisi wameteswa na utawala uliopita uliotokana na makabila mengine. Wanaamini kwamba hivi sasa ni zamu yao na Odinga ndiye mkombozi wao.
“Kwa ajili ya Wajaluo, Raila Odinga ndiye wanamuona atashughulikia udhalimu wanaoona kuwa wamefanyiwa,” anasema mmoja wa wachambuzi wa siasa za Kenya aliyezungumza na AFP kwa sharti la kutotajwa jina akirejea mauaji ya wanasiasa kadhaa kutoka jamii ya Wajaluo.
Familia ya Jaramogi
Odinga alipata urithi wa kisiasa kutoka kwa baba yake aliyeng’ara madarakani kabla ya kuangukia nje baada ya kutofautiana na Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta ambaye ni mzazi wa rais wa sasa.
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Odinga amefanya majaribio manne ya kushinda urais akilia kufanyiwa faulo kila alipopoteza.
Uchaguzi wa mwaka 2007 ulichochea unyanyasaji wa kikabila ambao uliwaacha watu 1,100 wakipoteza maisha na Odinga alidai kushinda. Rais wa wakati aliyekuwa akitetea nafasi yake, Mwai Kibaki alilazimika kuunda Serikali ya mseto iliyomhusisha Odinga na watu wake wa karibu.
Profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha St Lawrence kilichopo New York, Marekani anasema mpaka mwisho wa utawala wa kidemokrasia wa Rais mstaafu Daniel Arap Moi mwaka 2002 kulikuwa na ishara zilizoonekana kwamba, eneo la Nyanza lilikuwa kama limepigwa marufuku kwa miongo mingi kushika madaraka.
No comments:
Post a Comment