Baada ya Jaji John Mgeta aliyepangiwa kuisikiliza kesi hiyo upya kutoa uamuzi mdogo wa mabishano ya kisheria juu ya uamuzi huo wa majaji, bado upande wa Jamhuri umeamua kukata rufaa.
Raia wa Kenya, Samwel Saitoti na Peter Kimani wamehukumiwa kunyongwa wakati mshitakiwa Calist Kanje akihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kuwasaidia wakenya hao wasikamatwe na polisi.
Mauaji hayo ya Julai 11, 2007 yaliambatana na uporaji wa Sh239 milioni mali ya benki ya NMB tawi la Mwanga na PC Milanzi alikuwa lindo siku hiyo ya uporaji na kupigwa risasi hadi kufa.
Hata hivyo, walikata rufaa kupinga hukumu hiyo ya mwaka 2014 lakini jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa, Mbarouk Salum,Benard Luanda na Mussa Kipenga wakaamuru isikilizwe upya.
Majaji hao wamesema wamebaini katika mwenendo wa kesi hiyo iliyosikilizwa Moshi, wazee washauri wa mahakama hawakupewa nafasi inayostahili ili kuiwezesha mahakama kufikia maamuzi sahihi.
Wamesema katika shauri hilo, wamebaini makosa kadhaa ya kisheria na hivyo, wameagiza kufutwa mwenendo wote wa kesi na kesi hiyo kuanza upya kwa washitakiwa watatu waliokata rufaa.
Hata hivyo wakati kesi hiyo ikipangwa kuanza kusikilizwa upya jumanne iliyopita, kuiibuka hoja za kisheria kutoka kwa mawakili wa Serikali na wa utetezi na kuiomba mahakama kutoa mwongozo.
Upande wa Jamhuri ulihoji juu ya utata wa maagizo hayo ya majaji wa mahakama ya Rufaa kwa vile hayaelezi kama iwasilishwe hati mpya ya mashitaka au ibaki ile ya zamani yenye washitakiwa 12.
Pia akasema majaji walifuta mwenendo wa kesi tu lakini kutiwa kwao hatiani na adhabu waliyopewa hivyo hukumu ya awali bado inasimama na hivyo mahakama kuu haina tena mamlaka ya kuisikiliza.
Wakili wa Serikali mwandamizi Ladslaus Komanya, akasema kutokana na utata huo, haieleweke kesi hiyo ianze katika hatua ipi na kwa kutumia hati ipi wakati hukumu ya awali haikubatilishwa.
Wakili Majura Magafu anayemtetea Kanje kwa kusaidiana na wakili Erasto Kamani, alisema mteja wao alishamaliza kifungo chake Desemba 2016 na hakuna hati mpya ya mashitaka iliyowasilishwa kortini.
Kwa mujibu wa wakili Magafu, njia pekee ya kutatua mkwamo huo wa kisheria ni kwa Jaji Mgeta kuirudisha kesi hiyo kwa majaji watatu waliotoa maagizo hayo ili waipitie upya hukumu yao.
Hata hivyo wakili Allen Godian anayesaidiana na wakili Faustine Materu wanaowatetea raia hao wa Kenya, alikubaliana na amri ya majaji wa mahakama ya rufaa kuwa kesi hiyo ianze upya.
Katika hoja yake, wakili Godian alisema hukumu ya wateja wake ilitokana mwenendo wa kesi ambao umefutwa na mahakama ya rufani hivyo moja kwa moja hukumu nayo inakuwa imeondoka.
Akitoa uamuzi wake jana kuhusiana na mabishano hayo ya kisheria, Jaji Mgeta alikubaliana na hoja za wakili Godian akisema hakuna hukumu iliyosimama baada ya mwenendo wa kesi kufutwa.
Jaji Mgeta ametolea mfano wa nyumba akisema huwezi kuondoa msingi na paa likabaki hivyo akaagiza kesi hiyo ianze kusikilizwa upya kwa hati ya mashitaka ambayo tayari washitakiwa wanaijua.
“Nakataa pia wazo la mawakili la kupeleka kesi hii kwa majaji wa mahakama ya rufaa ili waipitie. Naagiza usikilizwaji upya uanze kwa kuanza kuchukua ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri,”amesema.
Mara baada ya Jaji kutoa uamuzi huo, wakili Komanya alisimama na kumueleza Jaji kuwa hawajaridhishwa na maamuzi hayo hivyo wameamua kuyakatia rufaa maamuzi yake madogo.
Wakili Magafu naye amesema nao walikuwa na nia ya kukata rufaa kuhusu kama mahakama ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, lakini watatoa hoja zao kupitia rufaa itakayokatwa na Jamhuri.
Jaji Mgeta amesema kukata rufaa ni haki ya kisheria hivyo nakala ya mwenendo wa shauri hilo na uamuzi wake mdogo zitakuwa tayari hiyo leo saa 9:00 jioni na kesi itatajwa Jumatatu.
No comments:
Post a Comment