Friday, November 3

Mwongozo mpya wa matumizi ya dawa mbioni kutolelewa



Naibu Waziri wa Afya Dk Faustine Ndugulile
Naibu Waziri wa Afya Dk Faustine Ndugulile 
Serikali kupitia Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto inatarajia kutoa mwongozo mpya wa matumizi ya dawa kabla ya mwaka huu kumalizika.
Naibu Waziri wa Afya Dk Faustine Ndugulile ameyasema hayo leo Novemba 3 wakati wa uzinduzi wa  cheti cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma katika kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015 kilichotolewa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Amesema mwongozo huo utasaidia kupunguza matumizi holela ya dawa ambayo mara nyingi huchangiwa na kampuni zinazozalisha dawa.
Amesema Serikali imeshaorodhesha jumla ya dawa muhimu 135 na inahakikisha dawa hizo zinapatikana kwa asilimia 80.
Dk Ndugulile  amesema serikali imeongeza bajeti ya fedha katika sekta ya afya kutoka Sh40 bilioni hadi Sh290 bilioni kuhakikisha zinakuwepo dawa za kutosha.
"Wafanyabiashara hasa wenye kampuni wamekua wakipita kwenye mahospitali kuhamasisha dawa ipi itumike, wao lengo lao ni kufanya biashara matokeo yake linakuja tatizo la usugu wa dawa,”
Amesema serikali itaendelea kusimamia kuhakikisha upatikanaji wa dawa haupungui.
Aidha Dk  Ndugulile ameitaka TFDA kuendelea kusimamia kwa ukamilifu uingizwaji wa dawa na vipodozi nchini.
"Hakuna asiyejua kuwa wote tunaguswa na kazi zinazofanywa na TFDA katika maisha ya kila siku. Hivyo kufanya vizuri kwa taasisi hii ni kuhakikishia umma kuwa afya zetu zinalindwa,"
"Niwasisitize msiridhike na mafanikio mliyoyapata mpaka sasa mnapaswa kukumbuka kuwa afya za watanzania zipo mikononi mwema, endeleeni kuboresha mifumo ya utendaji kazi,"
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo amesema mamlaka hiyo imekuwa ya kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki na ya pili Kusini mwa jangwa la sahara kupata cheti hicho.
Amesema cheti hicho imekipata baada ya kukidhi kiwango  kufuatia kufanyiwa ukaguzi na kampuni ya ACM Limited ya Uingereza.
Amesema mfumo wa uhakiki wa ubora wa huduma umesaidia kutengeneza, kufanya marejeo na kusimamia matumizi ya nyaraka, kufanya ukaguzi za ndani na kuratibu marejeo ya mfumo.

No comments:

Post a Comment