Wednesday, November 29

Serikali yahimiza waajiri kujiunga na Mfuko wa Fidia



Arusha. Serikali imewaagiza waajiri katika sekta binafsi na umma kujiunga na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kuchangia kuwawezesha wafanyakazi kupata mafao ya fidia wanapopatwa majanga ya ulemavu na ugonjwa unaosababishwa na kazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa WCF jijini Arusha.
Amesema leo Jumatano Novemba 29,2017 kuwa lengo la Serikali kuanzisha mfuko huo ni kuwawezesha kuwa salama na kunufaika na fidia wanapopatwa na matatizo.

Amesema Serikali itaendelea kuusaidia mfuko huo uweze kuwafikia wananchi wengi na hasa waajiriwa walio katika sekta za umma na binafsi.
Waziri Mhagama amesema ajali, maradhi na vifo vinasababisha kupunguza nguvu kazi mahala pa kazi na kurudisha nyuma juhudi za Serikali na sekta binafsi kuinua uchumi na kuongeza ustawi wa wafanyakazi.
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko wa WCF, Masha Mshomba amesema wataendelea kuboresha masilahi ya wafanyakazi ili watoe huduma bora kwa wafanyakazi waliopata majanga yaliyosababishwa na kazi zao.
Amesema mfuko unahakikisha wafanyakazi wanaoumia wanapata huduma bora na kurudi kazini haraka ili kuendelea kujenga uchumi wa nchi kwa gharama za mfuko.

No comments:

Post a Comment