The Hague, Uholanzi. Mahakama ya Kimataifa inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa watuhumiwa wa uhalifu wa iliyokuwa Yugoslavia ilisimama kwa muda ilipokuwa inasoma hukumu baada ya mshtakiwa kuonekana akinywa sumu kupinga kuridhiwa hukumu ya awali ya kifungo cha miaka 20 jela.
Majaji wa UN walikuwa wakisoma hukumu ya kesi za rufaa za viongozi sita wa zamani wa kisiasa na kijeshi wa Bosnia-Croatia, katika siku ya mwisho dhidi ya uhalifu wa kivita wa umwagaji damu uliofanywa wakati wakipigania kujitenga kutoka Yugoslavia miaka ya 1990.
Sekunde chache baada ya mahakama kukubaliana na hukumu ya awali, kamanda wa zamani wa jeshi Slobodan Praljak, 72, alisema kwa hasira: "Praljak siyo mhalifu. Napinga hukumu yenu."
Kisha aliinua kichupa kidogo na kukiweka mdomoni na kunywa kimiminika kilichokuwemo ndani huku kwa uwazi akipigwa picha za video zilizokuwa zikifuatilia usikilizwaji wa kesi hiyo.
Tukio hilo lisilo la kawaida lilikuja baada ya kuridhiwa hukumu ya kifungo cha miaka 25 dhidi ya Jadranko Prlic, waziri mkuu wa zamani wa taifa la Bosnia-Croatia lililokuwa likijitenga, na miaka 20 dhidi ya waziri wa ulinzi wa zamani Bruno Stojic.
Lakini usikilizwaji ulisitishwa haraka baada ya mwanasheria wa Praljak kupaza sauti akidai: "Mteja wangu amekunywa sumu."
Maofisa wa mahakama walipomzunguka Praljak mwenye madevu na mvi, jaji aliyeongoza usikilizwaji Carmel Agius ghafla aliamuru mchakato kusitishwa na mapazia yakashushwa kuzuia umaa kuona kinachoendelea.
Dakika chache baadaye waandishi wa shirika la AFP waliona gari la wagonjwa likiwasili nje ya mahakama wakati helikopta ikizunguka juu. Wafanyakazi kadhaa wa uokoaji walifika na vifaa. Baadaye mlinzi wa mahakama aliomba utulivu akisema Praljak alikuwa mzima “akipatiwa huduma muhimu."
Praljak alishtakiwa kwa kosa la kuamuru Novemba 1993 kuvunjwa kwa daraja la Mostar lililojenga karne ya 16, jambo ambalo majaji waliosikiliza kesi awali walisema “ilisababisha uharibifu usiomithilika kwa jamii ya Kiislamu ".
No comments:
Post a Comment