Wednesday, November 29

Rita waeleza changamoto utoaji vyeti vya kuzaliwa


Mtwara. Kukosekana huduma ya uhakika ya umeme na mtandao wa simu katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara ni moja ya changamoto zilizojitokeza katika usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Changamoto nyingine imetajwa ni uelewa mdogo wa wananchi wa kutotambua uhalali wa vyeti vilivyojazwa kwa mkono na baadhi ya watendaji kutoweza kutumia teknolojia ya simu katika kusajili.
Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Emmy Hudson amesema hayo leo Jumatano Novemba 29,2017 wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mpango wa usajili wa vizazi kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano.
Amesema mpango huo ulizinduliwa Septemba 26,2017 na kwamba wamesajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 276,623 sawa na asilimia 93.1 kutoka asilimia 10.4 kabla ya kuanza kwa mpango huo.
Hudson amesema watoto waliosajiliwa katika mkoani Lindi ni asilimia 96 kutoka asilimia 11.4 na kwa Mtwara ni asilimia 91.3 kutoka asilimia 9.4.
“Pamoja na mafanikio tuliyopata kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mitandao kwa sababu usajili unatumia teknolojia ya simu kwa hiyo kuna maeneo ya vijijini ambayo mtandao haupatikani inakuwa si rahisi kutuma taarifa kwenye kazi data ya Rita na kuchelewesha upatikanaji wa taarifa," amesema Hudson.
Amesema baadhi ya watendaji ni wazee walishindwa kutumia simu za kisasa (smartphone) ambazo ni vitendea kazi katika kuchukua na kuingiza taarifa kwenye kazi data ya Rita.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ameishauri Rita kushirikiana na taasisi za dini, kupata taarifa sahihi za watoto wanaozaliwa na kusogeza huduma katika ngazi za vijiji ili kuwafikia wanawake wanaojifungulia nyumbani.
Byakanwa alisema pamoja na kwamba huduma ya usajili na utoaji wa vyeti inafanyika katika ngazi za kata na vituo vya kutolea huduma ni vyema ikasogea na ngazi za vijijini.
Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa Rita, Hudson amesema mafanikio ya mpango huo yametokana na wadau wa maendeleo waliotoa michango likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef).

No comments:

Post a Comment