Saturday, November 11

Rais Magufuli aagiza barabara ya Mutukula-Minziro ijengwe


Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta fedha na kujenga barabara ya Mutukula – Minziro yenye urefu wa kilomita sita ili kurahisisha usafiri wa abiria na mizigo.
Agizo hilo amelitoa leo Jumamosi Novemba 11,2017 katika mji wa Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda baada ya kupokea kero za wananchi waliokusanyika jirani na geti la kuvuka mpaka huo.
Taarifa ya Ikulu imesema wananchi hao wamedai kukosekana kwa barabara hiyo kunawalazimu kuzunguka kwa kutumia barabara ya Kyaka.
Rais Magufuli pia amewataka viongozi wa Mkoa wa Kagera kufanyia kazi madai ya wananchi waliolalamikia kupata usumbufu katika kizuizi cha Kyaka jirani na Mto Kagera.
Hata hivyo, Rais amewataka wananchi wa Mutukula kutambua kazi ya ulinzi na usalama inayofanywa na vyombo vya dola. Pia, amewataka kutoa ushirikiano kwa viongozi na Serikali katika kuhakikisha mpaka huo unakuwa salama.
Amewataka wananchi kuongeza juhudi katika shughuli za maendeleo, zikiwemo za kilimo na biashara akirejea agizo lake la kuutaka Mkoa wa Kagera kujenga soko la kimataifa katika maeneo ya jirani na mpaka ili wananchi wapate mahali pa kuuzia bidhaa zao kwa njia halali.

No comments:

Post a Comment