Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa kuhakikisha kuwa uchaguzi mdogo wa madiwani utakaofanyika kesho (Jumapili) Novemba 22, 2017 unafanyika kwa amani na Utulivu.
Akisoma risala kwa umma leo Novemba 25 Jijini Arusha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa Wapiga Kura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga kura.
Amesema uchaguzi huo utakaofanyika katika kata 43 za Tanzania Bara, utakuwa na vituo 884 ambako ndipo wapiga kura wamejiandikishia kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2015.
Amesema kuwa tofauti na Chaguzi zilizopita, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuzingatia masharti ya sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa kifungu cha 62 imewaruhusu wapiga kura ambao ama kadi zao za kupigia kura zimepotea, kuchakaa au kufutika kutumia vitambulisho mbadala kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili waweze kupiga kura katika uchaguzi huu.
Jaji Kaijage amesisitiza kuwa masharti ya mpiga kura kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala yatazingatia sharti la kwamba majina ya mpiga kura lazima yafanane kwa herufi na majina yaliyoko katika kitambulisho mbadala ambayo yako katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Ameeleza kuwa katika kutekeleza hatua hiyo, vitambulisho mbadala ambavyo Tume ya Taifa ya uchaguzi imeruhusu vitumiwe na wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani ni leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya vitambulisho nchini (NIDA), pamoja na pasi ya kusafiria
Aidha, katika risala hiyo Jaji Kaijage amewataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika vituo vya kupigia kura kutoa kipaumbele kwa makundi maalum wakati wa kupiga kura.
Ameyataja makundi hayo kuwa ni wenye ulemavu wa aina mbalimbali, Wajawazito, Wenye watoto wachanga, Wazee na Wagonjwa.
Kuhusu Mawakala wa vyama vya siasa katika vituo vya Kupigia kura, Jaji Kaijage aliwasihi kufuata na kuzingatia, sheria kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika kipindi chote cha kupiga, kuhesabu na kujumlisha kura vituoni.
Aidha, Jaji Kaijage, amewataka Wananchi, wapenzi na Wakereketwa wa vyama kutofanya kampeni ya aina yeyote katika siku ya upigaji kura ikiwemo kusambaza vipeperushi, kuwa na bendera za Vyama vyao, na mavazi na kuwataka wananchi kuheshimu sheria za nchi wakati wote wa upigaji Kura, kuhesabu na kujumlisha kura.
No comments:
Post a Comment