Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameungana na wanafamilia na wananchi wa Songea kuomboleza kifo cha mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama, nyumbani kwa marehemu Likuyu Fusi wilayani Songea.
Majaliwa amesema alipokea taarifa za msiba huo kwa huzuni na mshtuko kwa sababu siku mbili kabla ya kuanza ziara mkoani Ruvuma, Gama alimpigia simu na kumjulisha kwamba anatangulia Songea ili kumpokea.
“Kifo ni mipango ya Mwenyezi Mungu, Gama ametangulia nasi tutafuata, hivyo wajibu wetu sote ni kumuombea. Gama alikuwa kiongozi na mwanga wa maendeleo,” amesema.
Gama amefariki dunia usiku wa kuamkia jana Ijumaa, Novemba 24,2017 katika Hospitali ya Misheni Peramiho mkoani Ruvuma alikokuwa akipatiwa matibabu na atazikwa Jumatatu, Novemba 27,2017 katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Likuyu Fusi.
Waziri mkuu Majaliwa amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa kifo cha Gama ni pigo kwa Serikali kwa sababu alishirikiana nayo tangu akiwa mtumishi wa umma na hata baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema msiba huo umeleta mtikisiko kwa sababu baada ya kurudi nchini kutoka India alikokuwa akipatiwa matibabu aliwaeleza kuwa hali yake ilikuwa nzuri.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme amemshukuru waziri mkuu kwa kutenga muda wa kwenda kuwafariji wafiwa licha ya majukumu mengi na makubwa aliyonayo.
No comments:
Post a Comment