Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa maandalizi ya vifaa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani unaofanyika katika kata 43 yamekamilika na awamu ya pili ya vifaa vitaanza kusafirishwa kesho Ijumaa kwenda katika kata husika.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Kailima Ramadhani, amesema leo Novemba 9 kwamba vifaa vitakavyosafirishwa kuanzia ni maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa vituo, makarani waongozaji pamoja na mfano wa karatasi za kupigia kura.
Amesema awamu ya kwanza ya kusafirisha vifaa ulifanywa na tume wakati wa mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi ambayo yalifanyika mjini Dodoma ambavyo vilitumika wakati wa uteuzi wa wagombea udiwani katika kata zote.
“Napenda kuwahakikishia umma kwamba tume imejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi huu na maandalizi ya kupeleka vifaa katika husika yako vizuri na awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa itapaelekwa Ijumaa ,”amesema Ramadhani.
Amesema awamu ya tatu ya usafirishaji wa vifaa itahusisha vifaa vichache ambavyo ni karatasi za kupigia kura pamoja na fomu za kutangazia washindi ngazi ya kituo na ngazi ya kata.
Naye Mkurugenzi wa Manunuzi, Ugavi na Logistiki wa NEC Eliud Njaila, amesema kwamba NEC imepeleka vifaa vya kutosha katika vituo vyote 893 vilivyoko katika kata 43 na hakutakuwa na upungufu wowote.
Amesema kwamba katika awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa, wameweka na mfano wa karatasi za kupigia kura ili wadau ambavyo ni vyama vya siasa vijiridhishe kuhusu karatasi hivyo zitakavyokuwa pamoja na kufanya uhakiki wa majina wa wagombea wao.
“Tunaamini kwamba vyama vya siasa vitahakiki majina ya wagombea wao kwa kila kata ili kama kuna masahihisho wayalete mapema na NEC iweze kufanya masahihisho haraka wakati wa kuchapa karatasi halisi za kupigia kura,” amesema Njaila.
No comments:
Post a Comment