Thursday, November 9

Kizza Besigye atumia medani kuwakwepa polisi


Kampala, Uganda. Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye ametumia medani kukwepa mtego wa polisi waliokuwa wamkamate baada ya kukaidi agizo lao.
Awali, mwanasiasa huyo alikaidi agizo la polisi waliomwamuru kuondoka katika eneo la viwanja vya Kuanda lililopo Manispaa ya Gulu.
Licha ya polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu, Besigye hakuwa tayari kuondoka.
Baada ya tafrani kupamba moto, Besigye alibadilisha gari na kupanda lingine aina ya Toyota Prado ambalo awali lilitumiwa na mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa chama chake cha FDC.
Kabla ya hatua hiyo, Besigye alikuwa ndani ya gari lake huku polisi wakiendelea kurusha mabomu ya kutoa machozi kwa lengo la kutaka kiongozi huyo kutoka ndani ya gari.
Baada ya kuona juhudi za kumwondoa zimeshindikana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Aswa aliwaamuru askari kulikamata gari lake na kulipeleka kituo cha Guru.
Askari walipojaribu kuzuia gari la kiongozi huyo, alikuwa tayari ameondoka eneo la tukio akielekea mjini Kampala.
Katibu wa uenezi wa chama cha  FDC, Kelly Komakech aliliambia gazeti la Daily Monitor kuwa polisi hawakujua gari lililombeba Besigye na jinsi lilivyoondoka.
“Besigye aliondoka na kuwashinda askari. Walijaribu kumfuata lakini hawakuweza,” alisema.
Hata hivyo, msemaji wa polisi, Jimmy Okema alipuuza madai ya polisi kupigwa chenga na Besigye akisema walikubaliana kiongozi huyo aondoke katika eneo hilo.
Mwanasiasa huyo aliyewania urais kwa mara nne alikuwa ameambatana na viongozi wengine kadhaa wa chama chake kwa ajili ya mkutano ambao polisi walisema haikuwa halali.

No comments:

Post a Comment