Saturday, November 4

Madaktari wa kujitolea wa China kuendelea kufanya kazi nchini


Dar es Salaam. Balozi wa China nchini, Wang Ke amesema Watanzania 15.2 milioni wametibiwa na madaktari wa kujitolea wa Taifa hilo ambao wamekuwa wakifika Tanzania tangu mwaka 1968.
Akizungumza jana Ijumaa Novemba 3,2017 wakati wa kuwaaga madaktari waliokuwepo nchini kwa miaka miwili, Balozi Wang amesema hilo ni kundi la 24 la madaktari kuingia nchini tangu mpango huo ulipoanza na wataendelea kuwaleta wengine.
Amesema madaktari hao wamekuwa wakitoa huduma wakisaidiana na wenzao wa Tanzania katika hospitali za Muhimbili, Dodoma, Tabora na Musoma.
Balozi Wang amesema madaktari hao 25 wamebobea katika magonjwa mbalimbali ukiwemo wa moyo.
"Mbali na kuhudumu katika hospitali hizo, walikwenda vijijini kuwafuata wagonjwa na kuwahudumia,” amesema.
Amesema katika awamu ya 24, madaktari hao wametoa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh125 milioni.
Balozi Wang amesema baada ya madaktari hao kuondoka, watakuja wengine kwa kuwa mpango huo ni endelevu.
"Tutaendelea kuleta madaktari ili washirikiane na wenzao wa Tanzania kwa lengo la kuwapatia uzoefu," amesema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha wagonjwa wote wanatibiwa nchini badala ya kuwapeleka nje ya nchi.
Amesema ili kufanikisha lengo hilo, Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali za kanda zinahitaji kuboresha huduma zake.
Mwalimu amesema ndiyo maana Serikali imeiomba China madaktari 11 ambao watafanya kazi Muhimbili, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa Mbeya na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
"Tunashukuru kwa kutupatia madaktari hawa na tunatarajia Serikali ya China itaendelea kutusaidia wataalamu zaidi wa afya," amesema.
Waziri Mwalimu amesema mpango wa madaktari wa kujitolea kuja nchini umepunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda nje kutibiwa.
Kiongozi wa madaktari hao, Dk Sun Long amesema kwa miaka miwili waliyokaa Tanzania wamewapa uzoefu wenzao waliopo nchini.
Dk Sun ambaye ni daktari wa upasuaji wa moyo amesema madaktari wa moyo ni wachache Tanzania, hivyo ameshauri wasomeshwe wataalamu wa aina hiyo.

No comments:

Post a Comment