Patrice Evra ambaye kwa sasa huchezea Marseille ya Ufaransa alifukuzwa uwanjani baada ya kumshambulia mmoja wa mashabiki wa timu hiyo wakati wa kujiandaa kwa mechi.
Evra alimpiga kichwani shabiki wachezaji wakipasha misuli moto uwanjani kabla ya kuanza kwa mechi ya ugenini dhidi ya Vitoria Guimaraes katika ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League.
Marseille walilazwa 1-0 mechi hiyo.
Picha za video zinamuonesha mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United mwenye miaka 36 akiruka juu na kumpiga teke shabiki huyo.
Evra, ambaye alikuwa ametajwa kwenye benchi, alifukuzwa uwanjani hata kabla ya mechi kuanza.
Marseille walianza wakiwa na wachezaji 11.
Shirikisho la soka Ulaya Uefa limemfungulia mashtaka ya kufanya kitendo cha ghasia.
Amesimamishwa kucheza "angalau mechi moja" huku Uefa wakitarajiwa kuamua hatima yake 10 Novemba.
Gazeti la Ufaransa la L'Equipe limesema mashabiki wa Marseille walikuwa wamemzomea Evra kwa karibu nusu saa wachezaji walipokuwa wakijiandaa kwa mechi.
Evra alikuwa ameenda kuzungumza nao kuwatuliza lakini badala ya kupunguza kelele, wakazidisha na hali ikabadilika ghafla.
Mwanahabari wa Ufaransa Julien Laurens amesema Evra - ambaye mara nyingi hupakia video za ucheshi kwenye mitandao ya kijamii - alitukanwa na kuambiwa: "Endelea kuandaa na kusambaza video zako, lakini uache kucheza kandanda."
Marseille wamesema wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho na kusisitiza kwamba mchezaji wakati wowote anafaa kujituliza hata anapozomewa au kurushiwa matusi.
Kisa hicho kimewakumbusha wengi kuhusu "kiki cha kung-fu" ya Eric Cantona wakati wa mechi kati ya Manchester United na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park Januari 1995.
Mfaransa huyo alipigwa marufuku miezi tisa na Chama cha Soka cha England kutokana na kisa hicho ambacho kilitokea alipokuwa akiondoka uwanjani baada ya kulishwa kadi nyekundu.
No comments:
Post a Comment