Saturday, November 4

Mgogoro wa madiwani, DC kupima uwezo wa waziri



Naibu waziri wa Tamisemi, Joseph Kakunda
Naibu waziri wa Tamisemi, Joseph Kakunda 
Tunduma. Mgogoro wa madiwani wa Halmashauri ya Tunduma na mkuu wa Wilaya ya Momba, Jumaa Irando umezidi kuwa mwiba kwa Serikali baada ya naibu waziri wa Tamisemi, Joseph Kakunda kufika mjini hapa na kusikiliza hoja za pande zote lakini akashindwa kutoa uamuzi.
Hata hivyo, Kakunda katika kikao kilichofanyika faragha bila kuhusisha vyombo vya habari, aliahidi kutoa uamuzi wa mgogoro huo kabla ya Novemba 6.
Mgogoro huo ulianza baada ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Mwafongo na mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajoka kutangaza hadharani kuondoa ushirikiano na Irando kuanzia kwa wenyeviti wa Serikali za mitaa kwa madai amekuwa akiingilia na kuchukua uamuzi kwa kutumia ubabe.
Hata hivyo, baada ya tamko hilo ambalo lilitolewa na Mwafongo katika mkutano wa hadhara mjini Tunduma Agosti 18, Irando naye akajibu mapigo kwa kuandika waraka maalumu kwa watendaji wote wa Serikali kutopokea maelekezo wala amri yoyote kutoka kwa madiwani hao. Pia, alifuta vikao vyote vya baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
RC anyanyua mikono
Mgogoro baina ya vigogo hao umefikia hatua ya kukosa ufumbuzi wa kudumu baada ya mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa naye kuonekana kushindwa kuutatua na kuamua kuitupia ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Jumatatu ya wiki hii, naibu waziri huyo alilieleza gazeti hili kuhusiana na safari yake Tunduma kuwa, mgogoro wa viongozi hao ni mkubwa na unahitaji umakini na busara zaidi katika kuupatia ufumbuzi.
Jumanne, Kakunda alifika Tunduma na kufanya kikao cha faragha kusikiliza hoja za pande zote.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kilichoamriwa na Kakunda baada ya kikao hicho, mkuu wa wilaya hiyo Irando na Mwafongo walisema kila upande ulipata nafasi ya kutoa hoja zake lakini hawakupewa uamuzi papo hapo.
Irando aliliambia gazeti hili kuwa Kakunda alisikiliza hoja za madiwani kwa kuwa taarifa zake (Irando) alishaziwasilisha wizarani muda mrefu. “Kwa upande wangu taarifa anazo kwa kuwa tulishapeleka muda mrefu hivyo hapa alikuwa anawasikiliza madiwani, tunasubiri jibu la uamuzi utakaoamriwa, ila sisi tunaendelea kuchapa kazi na mambo yapo vilevile,” alisema.
Naye Mwafongo alisema walitoa hoja zao katika kikao hicho huku akimshukuru Kakunda kwa kuwasikiliza kwa utulivu na kutoa ahadi ya kutoa suluhisho la mgogoro huo kabla ya Novemba 6.
“Kinachoonekana hapa kulikuwa na taarifa tofauti kuhusu mgogoro huu, tulitangaza kuondoa ushirikiano na Irando (mkuu wa wilaya) kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake wa kibabe, hivyo tunaona hatoshi katika wadhifa wake lakini hatukusema hatuitambui Serikali kama wanavyodai,” alisema Mwafongo.
Alisema madiwani kupitia baraza lao wataendelea kufanya kazi za kuishauri Serikali kwa mustakabali wa maendeleo ya wananchi, lakini wanapoona mtu mmoja ama kikundi kinataka kufanya jambo kinyume na matarajio ya wengi watapaza sauti kwa kufuata taratibu zinatotakiwa.

No comments:

Post a Comment