Wanajeshi wa Zimbabwe wamemuweka rais Mugabe kwenye kizuizi cha nyumbani hatua inayoonekana kuwa wametwaa mamlaka ya nchi. Meja jenerali Sibusiso Moyo amesema lengo ni kuwakabili wahalifu wanaomzunguuka rais Mugabe.
Meja jenerali Moyo pia amefahamisha kuwa rais Mugabe na familia yake wako salama salimini na kwamba watahakikishiwa usalama wao. Na kwa mujibu wa taarifa kutoka Afrika Kusini kiongozi wa nchi hiyo rais Jacob Zuma alizungumza na rais Mugabe mapema jana na kuthibitisha kwamba kiongozi huyo wa Zimbabwe amewekwa kwenye kizuizi cha nyumbani kwake. Rais Zuma alisema baadaye kwamba amewapeleka wajumbe nchini Zimbabwe.
Taarifa zaidi zinasema afisa mmoja wa Zimbabwe ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba waziri wa fedha Ignatius Chombo pia amewekwa mahabusu. Magari ya kijeshi na vifaru yalionekana kwenye mitaa ya mji mkuu Harare huku milio ya risasi ikisikika katika vitongoji vya kaskazini mwa mji huo ambako rais Mugabe na viongozi wengine wa serikali ya Zimbabwe wanaishi.
Wanajeshi wa Zimbabwe wametwaa mamlaka wiki moja baada ya rais Mugabe kumfukuza kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa. Mwanasiasa huyo alifukuzwa baada ya mke wa Mugabe, Grace, kumwambia mumewe. Mnangagwa na mkuu wa jeshi la Zimbawe jenerali Constantino Chiwenga aliyeongoza hatua za kijeshi za kutwaa mamlaka ni washirika walioshiriki pamoja katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe. Licha ya wanajeshi kukanusha kwamba wamepindua serikali wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua walizochukua zinaonyesha ishara zote za kuangushwa kwa serikali ya rais Mugabe.
Wanajeshi walikitwaa kituo cha utangazaji cha serikali na jenerali alionekana kwenye televisheni kutangaza kutwaa mamlaka. Magari ya kijeshi yaliifunga barabara inayoelekea kwenye ofisi muhimu za serikali, bunge na mahakama katikati ya mji wa Harare hata hivyo hali ilionekana kuwa tulivu katika mji mkuu huo.
Katika mawasiliano ya kwanza ya nje tangu wanajeshi walipotwaa mamlaka rais Mugabe alizungumza kwa njia ya simu na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na kumwambia kwamba amewekwa kizuizini nyumbani kwake lakini yuko salama. Haijawa wazi iwapo hatua iliyochukuliwa na wanajeshi inaashiria mwisho wa utawala wa Mugabe ambaye sasa ana umri wa miaka 93. Waziri wa ulinzi na mwenzake wa usalama wa Afrika Kusini wamekwenda Harare kujaribu kuanzisha mazungumzo baina ya rais Mugabe na majenerali wa jeshi la nchi hiyo taarifa hiyo imetolewa na vyombo vya habari vya Afrika Kusini bila ya kufafanua zaidi.
Akizungumzia juu ya hali ya Zimbabwe katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito wa utulivu na subira nchini. Msemaji wa Guterres ameeleza kuwa katibu mkuu huyo amesisitiza umuhimu wa kulinda haki za kimsingi ikiwa ni pamoja na uhuru wa kutoa maoni na kufanya mikutano. Naye Rais wa Umoja wa Afrika Alpha Conde amelaani hatua ya wanajeshi wa Zimbabwe ya kutwaa mamlaka ya nchi hiyo amewataka wanajeshi hao warejee kambini ili kuiheshimu katiba. Conde amesema atazungumza na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ili kuanzisha mawsiliano na rais Mugabe.
Wakati hayo yakijiri kiongozi wa tawi la vijana la chama tawala cha ZANU-PF Kudzai Chipanga amewaomba radhi wanajeshi kwa kumdharau mkuu wa majeshi jenerali Constantino Chiwenga. Hapo awali alimlaumu jenerali huyo kwa kuhujumu katiba ya Zimbabwe. Tawi hilo la vijana wa chama tawala limekuwa linawaunga mkono thabiti rais Mugabe na mkewe Grace.
Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change MDC kimetoa mwito wa kurejea kwenye utaratibu wa katiba na demokrasia kwa njia ya amani. Chama hicho kimeeleza matumaini kwamba hatua zilizochukuliwa na wanajeshi zitaweka msingi wa kuanzishwa nchi imara ya kidemokrasia.
No comments:
Post a Comment