Mwanza. Katika kampeni za lala salama leo, CCM itawapandisha jukwaani aliyekuwa mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi na Dk Louis Shika, aliyejizolea umaarufu baada ya kuibuka kwenye mnada wa nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi.
Katambi aliyejiunga na CCM akitokea Chadema na Dk Shika watamnadi kwa wapiga kura wa Kata ya Mhandu jijini Mwanza mgombea wake, Constantine Sima.
Katibu wa uenezi wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Mustapha Banigwa amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa wengine watakaopanda jukwaani katika mkutano utakaofanyika mtaa wa Machinjioni ni waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi na mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha aliyerejea CCM akitokea Chadema.
Mkutano huo pia utahutubiwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa mbunge wa Bunda, Stephen Wasira, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na mbunge wa Bukombe, Doto Biteko.
Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 nchini utafanyika kesho Jumapili Novemba 26,2017.
No comments:
Post a Comment