Saturday, November 25

Makamishna wakana ulaghai uchaguzi Liberia


Monrovia, Liberia. Bodi ya makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetupilia mbali wito wa vyama vya Unity na Liberty wa kutaka uchaguzi mkuu wa Oktoba 10 urudiwe ikisisitiza vyama hivyo vimeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha juu ya madai ya udanganyifu na dosari.
Mahakama ya Juu ya Liberia mwezi uliopita ilizuia kura ya marudio kwa wagombea wawili wa mwanzo ambayo awali ilipangwa kufanyika Novemba 7, hadi Bodi ya NEC itakapokuwa imesikiliza malalamiko yaliyowasilishwa na Liberty.
Katika uamuzi wake Ijumaa, Bodi ya Mkamishna imekazia uamuzi uliotolewa na Ofisa wa NEC aliyesikiliza shauri kwamba vyama viwili hivyo vimeshindwa kuthibitisha ulivyofanyika udanganyifu.
“Mahakama ya Juu imefafanua udanganyifu kuwa ni matumizi ya hila, usanii, hadaa na ulaghai au upotoshaji na kwa hiyo haitoshi tu kudai udanganyifu kama msingi wa kujipa faraja, lazima uthibitishwe kwa ushahidi,” alisema Kmishna Davidetta Lassanah aliyesoma uamuzi kwa niaba ya Bodi.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, imekubaliwa kwamba yalifanyika makosa ya ubadilishaji katika uchaguzi wa Oktoba 10 lakini yalirekebishwa na hayakuwa na athari kwa matokeo yote ya ujumla wala kustahili kuitwa ni udanganyifu.
“Kwa hiyo, tunasisitiza kwamba Ofisa wa NEC aliyesikiliza shauri hakukosea, na tunakataa ombi la mlalamikaji wa kwanza na wa pili kutaka uchaguzi wa Oktoba 10, 2017 urudiwe.
Kwa sababu hiyo na kwa mtazamo wa maelezo ya hapo awali, wito wa walalamikaji umekataliwa. Uamuzi wa mwisho wa Ofisa Msikilizaji wa mchakato huu umethibitishwa na umeridhiwa na kwa hiyo imaamliwa hivyo,” alisema
Wanasheria wa vyama hivyo vya siasa walichukua nukuu kadhaa katika uamuzi huo na wakatangaza kwenda Mahakama ya Juu kukara rufaa.

No comments:

Post a Comment