Saturday, November 11

Dk Shika awa gumzo mtandaoni


Dar es Salaam. Wakati Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ikiendelea kumshikilia Dk Louis Shika kwa tuhuma za kuharibu mnada wa nyumba za mfanyabiashara maarufu Said Lugumi, mijadala kuhusu mteja huyo imeendelea kwenye mitandao ya kijamii.
Novemba 9,2017 kampuni ya udalali ya Yono kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendesha mnada wa nyumba za Lugumi mbili za Mbweni JKT na moja Upanga jijini Dar es Salaam ambazo zote Dk Shika alifikia bei ya kuzinunua kwa Sh3.2 bilioni.
Hata hivyo, Dk Shika amejikuta akiishia mikononi mwa vyombo vya dola baada ya kushindwa kulipa asilimia 25 ya fedha hizo. Nyumba za Mbweni JKT alifika bei kwa Sh900 milioni na nyingine Sh1.1 bilioni, huku ya Upanga alifika bei ya Sh1.2 bilioni.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema, ‘’Tunaendelea kumshikilia na Jumatatu –Novemba 13,2017 kama jalada litakuwa limerudi kutoka kwa mwanasheria wa Serikali tutamfikisha mahakamani.”
Mwonekano wa mavazi, mazungumzo yake na jinsi alivyofika Mbweni JKT uliwatia shaka baadhi ya watu kama kweli Dk Shika amedhamiria kununua nyumba hizo au katumwa na mtu kufanya hizo.
Dk Shika alifika Mbweni kulikofanyika mnada wa nyumba mbili akitumia pikipiki ‘bodaboda’ na alipoulizwa na Mwananchi ametokea wapi na kama ana gari, alisema hana gari kwa kuwa ameingia nchini hivi karibuni akitokea ughaibuni kwa shughuli hiyo ya mnada na anaishi Kigamboni na Tabata Mawenzi.
Katika mitandao ya kijamii tangu Novemba 9,2017 Dk Shika anaendelea kujadiliwa, huku wengine wakitumia picha zake kumjadili wakiziambatanisha na ujumbe mbalimbali.
Ujumbe mwingine unaosambaa ni ule unaoonyesha jinsi alivyokuwa akipandisha bei kushindana na wenzake baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Yono, Scholastica Kevela kutangaza kufungua mnada.
“Mteja atakayefika bei, atatakiwa kulipa leoleo asilimia 25 ya gharama itakayofikia,” alisema Scholastica akifungua mnada na kutaka mwenye ofa kuanza.
Mmoja wa wateja alijitokeza akisema atatoa Sh300 milioni lakini Dk Shika alisema mia tatu hamsini, mwingine akasema mia nne, Dk Shika akasema mia tano lakini baada ya kufikia mia 700, Dk Shika alisema, “Mia tisa itapendekeza sana.’’
Bei hiyo haikufikiwa na mwingine, hivyo alitangazwa mshindi.

No comments:

Post a Comment